SWALI
Nawashukuru
mashehe wetu kutujibia masuali kwani hatuna pengine pa kuuliza hasa
huku nchi za nje ni shida kupata mtu wa kuuliza masuali hivo tunafanya
mambo bila kujua ipasavo. Mungu awalipe mema mingi mzidi kutuhudumia na
kutuelemisha.
Nauliza
kuhusu suna za ijumaa napokwenda kusali msikitini je, nisali kwanza
tahiya ya masjid, kisha nisali tena zile suna za kablia 4 na baada ya sala nisali zile 2 za baadia? Maana nimesikia hakuna haja kusali suna siku ya ijumaa.
Na je ikiwa nasali nyumbani hiyo sala ya ijuma inakuwaje hizo suna nisali vipi? Asanteni sana.
JIBU:
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Shukrani zetu za dhati kwa ndugu yetu muulizaji swali. Awali ya
yote ni kuwa si kweli kuwa hakuna Swalah za Sunnah kabla ya Swalah ya
Ijumaa. Kisha ni kuwa pindi anapoingia Msikitini siku ya Ijumaa anafaa
mtu aswali Sunnatut Tahiyyatul Masjid (Sunnah ya kuusalimu Msikiti).
Sunnah hii ni muhimu na inafaa itekelezwe hata kama Imaam tayari amepanda juu ya Minbar na anahutubu inafaa uiswali kwa kuifanya wepesi na si kurefusha (Muslim na Ahmad).
Mbali
na hiyo Sunnah, Muislamu akifika mapema anaweza kuswali idadi yoyote
anayoweza yeye bila kuikalifisha. Hiyo ni kwa mujibu wa Hadiyth: “… kisha akaswali kiasi chake…” (Al-Bukhaariy
na Ahmad). Hii ni sehemu ya Hadiyth ndefu yenye adabu za mtu
anayejitayarisha kwenda Msikitini siku ya Ijumaa mpaka kumalizika kwa
Swalah yenyewe.
Shaykh al-Islaam Ibn Taymiyyah (Allaah Amrehemu) amesema: “Ni bora kwa anayekwenda kwenye Swalah ya Ijumaa ajishughulishe na kuswali mpaka afike Imaam kama ilivyo katika kauli ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): ‘Kisha anaswali aliyoandikiwa’ (al-Bukhaariy kutoka kwa Salmaan al-Faarisiy [Radhiya Allaahu ‘anhu]).
Katika
athari za Maswahaba (Radhiya Allaahu ‘anhum) ni kuwa walipofika
Msikitini Ijumaa wanaswali walivyoweza, wapo waliokuwa wakiswali rakaa
10, wengine 12 na wengine 8 na wengine chini ya hapo. Hivyo, wamesema
wengi miongoni mwa ma-Imaam kuwa hakuna kabla ya Ijumaa idadi maalumu za
Sunnah” (Dkt. Swaalih Fawzaan, al-Mulakhkhasw al-Fiqhiy, Mj. 1, uk. 250
– 251 kutoka kitabu cha Fataawa).
Ama
baada ya Swalah ya Ijumaa unaweza kuswali mbili au nne. Ataswali nne
hapo hapo msikitini, au ataswali mbili atakaporudi nyumbani kwake. Zote
zimethibiti kwenye Hadiyth sahihi za Mtume (Swallaa Allaahu ‘alayhi wa
aalihi wa sallam) kama zifuatavyo:
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Akiswali mmoja wenu Ijumaa, aswali baada yake nne” (Muslim kutoka kwa Abu Hurayrah [Radhiya Allaahu ‘anhu]).
Na Ibn ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhuma) amesema: “Hakika yeye (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiswali baada ya Ijumaa Rak’ah mbili” (al-Bukhaariy na Muslim).
Swalah
ya Ijumaa inaswaliwa Msikitini peke yake. Ikiwa kwa sababu moja au
nyingine hukuweza kuiswali Msikitini basi inafaa kwako uswali Swalah ya
Adhuhuri. Ikiwa utaswali Swalah ya Adhuhuri huko nyumbani utaswali
Sunnah za kawaida – kabla Rak’ah nne na baada Rak’ah mbili.
0 comments:
Post a Comment