Makala ya Fiqh
.Kuna makosa yanayofanyika
katika uletaji wa Sijida Sahau (Sujud as-Sahw)
.Zipo sijda sahau zinazoletwa
baada ya kutoa salamu, na zipo za kabla ya salamu
.Iwapo umechelewa kuunga
Swala, na Imamu kaleta sijidasahau ufanyeje?
(Na Omar Haliim, Mfasiri S.
Hussein)
Uko katika Swala lakini unapitiwa. Unahisi sijui umeacha jambo fulani,
sijui umelifanya. Unakata shauri bora usahihishe kosa kwa kuleta sijida mbili
baada ya Swala ili kufidia upungufu huo. Lakini je unafanya jambo hilo kabla ya
kumaliza Swala au baada? Je tendo hilo linafidia makosa yote katika Swala, au
baadhi tu? Je inakuwaje pale wewe unapopitiwa na jambo fulani katika Swala
lakini Imamu unayemfuata hakupitiwa? Je inakuwaje iwapo utakumbuka kosa baadae
ukiwa umeshamaliza Swala?
Wengi wetu tunaijua sijida sahau (Sujud as Sahw). Lakini wengi wetu
hatuzijui hukumu zinazohusiana na Sijida hiyo. Hivyo, imekuwa kawaida kufanya makosa
katika sijida hiyo.
Miaka kadhaa iliyopita, Sheikh Mashuhuri Muhammad ibn Saleh al-Uthaymiin
(d.1421/2001) aliandika kijitabu kimoja kizuri sana juu ya suala hili ili
kufafanua matumizi na masharti ya Sijida Sahau. Hii, kwa mukhtasari,
inafafanuliwa kama ifuatavyo.
Neno Sahw la Kiarabu lina maana ya ‘kupitiwa’, ‘kughafilika’ au ‘kusahau’.
Sujud as-Sahw ni sijida mbili ambazo mtu huzileta mwishoni mwa Swala ili
kufidia kosa. Kuna sababu tatu ambazo Sijida Sahau hufanyika kwazo:
1.
Kuongeza jambo katika Swala ambalo halikuagizwa
2.
Kusahau kufanya jambo lililoagizwa
3.
Kuwa na shaka (hatihati) kama umefanya kosa fulani au la.
Makosa ya Kuzidisha
1. Kuzidisha Rakaa
Iwapo mtu anayeswali, anazidisha kwa makusudi jambo fulani ambalo
limeagizwa katika Swala kama vile kuongeza sijida moja zaidi, basi kitendo
hicho hakijuzu, ni batili. Iwapo mtu anazidisha jambo kwa bahati mbaya, basi
Swala yake inajuzu, ila ni lazima alete Sijida-sahau (sujud as-Sahw). Iwapo mtu katanabahi kuwa kafanya kosa wakati bado
akiwa ndani ya Swala, basi lazima arudi katika kitendo sahihi cha Swala.
Mathalani, kama mtu anaswali Dhuhuri kisha akatanabahi kuwa kazidisha
rakaa, kwamba sasa yupo katika rakaa ya tano, basi arudi moja kwa moja katika
kikao (jalsa) cha tahiyatu na atimize utaratibu wa shahada (tashah-hud).
Na iwapo hakuweza kutambua kosa hadi baada ya kuwa ameshamaliza Swala, au
baada ya kuwa amemaliza jambo ambalo halikuagizwa katika Swala, basi alete tu
Sijida Sahau. Hii ni hukumu ya mtu ambaye kaswali dhudhuri kwa rakaa tano
ambaye katambua kosa baada ya kutimiza shahada.
Katika hali zote hizo mbili, sijida sahau huletwa baada ya tasliim (kutoa
salamu mwishoni mwa Swala) kwa sababu hili ni kosa la kuzidisha jambo katika
Swala. Uthibitisho wa Hukumu hii ni Hadith ya Mtume, swallallahu alayhi wa
sallam, iliyosimuliwa na Bukhari na Muslim kwa mapokeo ya Ibn Masoud kwamba
Mtume, swallallahu alayhi wa sallam, aliwahi kuswali dhuhuri kwa rakaa tano,
ambapo ikaulizwa, “je Swala imezidishwa?’ Mtume, Swallallahu alayhi wa sallam,
akauliza, “kwa nini iwe hivyo?” Maswahaba wakasema, ‘Uliswali rakaa tano.’ Basi
Mtume, swallallahu alayhi wa sallam akaleta Sijida Sahau.
2. Kutoa Salamu Kabla ya Kumaliza
Swala
Kutoa salamu na kumaliza Swala kabla haijakamilika kunahesabiwa kama ni
kuongeza kitu katika Swala kutokana na mtazamo kuwa Swala imetiwa salamu ya
nyongeza. Kama kitendo hicho kimefanyika kwa makusudi basi Swala haiswihi.
Lakini kikifanyika bila kujua yaani yule anayeswali hakutambua kuwa kamaliza
Swala kabla ya kufika mwisho wake, na hata ukapita muda mchache, basi huyu
airudie Swala kuanzia mwanzo kabisa. (Muda mchache hapa una maana ya zaidi ya
dakika chache).
Hata hivyo, iwapo kakumbuka kosa lake muda mfupi baada ya kutoa salamu,
basi akamilishe Swala na kisha baada ya kutoa salamu mwishoni mwa swala hiyo
ndipo sasa alete Sijida sahau.
Uthibitisho wa hukumu hiyo ni Hadith ya Mtume, swallallahu alayhi wa sallam, iliyosimuliwa na Bukhari na Muslim
kwa mapokeo ya Abu Hurayrah. Mtume, swallallahu alayhi wa sallam, aliwaswalisha
Maswahaba ama Dhuhur au Asri na akatoa salamu baada ya rakaa mbili....Basi mtu
mmoja akasimama na kusema: “Ewe Mtume wa Allah!Ulipitiwa au Swala imefupishwa?”
Mtume, swallallahu alayhi wa sallam, akasema, “Si hivyo wala hivyo.” Mtu huyo
akasema, “Hapana, hakika umepitiwa.” Ndipo Mtume, swallallahu alayhi wa sallam,
alipowauliza Maswahaba wake, “Je ni kweli anavyosema?” Wakajibu, “Ndiyo” Basi
Mtume, swalallahu alayhi wa sallam, akainuka na kumalizia sehemu aliyoacha ya
Swala, akatoa salamu, akaleta Sijida Sahau, kisha akatoa tena salamu.
Iwapo Imamu katoa salamu kabla swala haijakamilika sawasawa, huku kukiwa na
watu wanaomfuata ambao wamekosa sehemu ya Swala, na papo hapo Imamu akakumbuka
kosa lake baada ya wale waliochelewa Swala kuwa tayari wameshasimama kumalizia
sehemu waliyoikosa, basi wachelewaji wana hiyari ama kumalizia Swala na kuleta
Sijida sahau (kila mmoja na yake mwenyewe) baada ya kutoa salamu, au kumfuata
Imam na kisha baada ya Imamu kutoa salamu wamalizie sehemu waliyoikosa, lakini
hiyo iwe kabla Imamu hajaleta Sijda sahau. Kisha wachelewaji baada ya kumaliza
sehemu waliyokosa, nao walete Sijida sahau na kisha watoe salamu. Rai hii ya
pili ndiyo iliyopendelewa. Sababu ya wachelewaji kutoswali sijida sahau na
Imamu ni kwamba pale Imamu anapomaliza swala kwanza na kisha kuleta sijida
sahau, hawa wachelewaji wanazuilika kumaliza swala yao pamoja na Imamu kwani
bado haijakamilika.
Makosa ya Kupunguza
Kuhusiana na makosa ya Swalan yanayohusu kuacha sehemu ya nguzo ya Swala,
hukumu ni hizi:
1. Nguzo
Iwapo takbira ya kuhirimia (takbira ya kwanza) inayomwingiza mtu katika
Swala (takbiirat-ul-ihram) inaachwa,
ama kwa makusudi au kwa bahati mbaya, Swala haiswihi. Iwapo nguzo ya Swala
inaachwa kwa kughafilika au kwa kupitiwa huku yule anayeswali akishindwa
kutanabahi kwa kosa lake hadi akafika mahali palepale alipopaacha katika rakaa
ya kwanza wakati akiwa katika rakaa iliyofuata, basi rakaa ya kwanza inahesabiwa
kuwa imetenguliwa, na hivyo, hii ya pili inachukua nafasi yake bila mtu
kufungua Swala au kuanza upya. Iwapo mtu anatambua kosa lake na yupo
katika rakaa ya pili lakini bado
hajafika ile sehemu aliyoikosea katika rakaa ya kwanza, basi papohapo mtu huyo arudi
kwenye nguzo, aitimize, kisha aendelee na Swala kuanzia hapo. Katika hali zote
hizo mbili sijida sahau inakuja baada ya kutoa salamu kwa sababu kuna mambo
yaliyoongezwa ndani ya Swala.
Mfano wa kadhia ya kwanza ni huu: Mtu kasahau sijida ya pili katika rakaa
ya kwanza lakini kashindwa kutanabahi hadi akafika katika tahiyatu (jalsa) ya
rakaa ya pili. Katika hali hii, ile rakaa ya kwanza haihesabiwi tena na badala
yake rakaa hiyo ya pili ndiyo inayochukua nafasi yake. Mtu aendelee na rakaa
hiyo (yaani aendelee kuitimiza), lakini sasa ajue kuwa hiyo ndiyo rakaa ya
kwanza, na inayofuata ndio itakuwa ya pili na kuendelea.
Mfano wa kadhia ya pili waweza kuwa kama ifuatayo: Mtu kasahau sijida ya
pili pamoja na kikao (jalsah) kinachoitangulia na akakumbuka kuwa kaacha hayo
baada ya kuwa ameitidali (ameinuka kutoka kwenye rukuu) ya rakaa iliyofuata,
katika hali hii, mtu lazima atoke moja kwa moja kwenye itidali na kurudi kwenye
kikao alichoacha na aendelee na Swala kuanzia hapo. Kisha baada ya kumaliza
Swala alete Sijda sahau, kwa sababu kuna mambo yameongezwa.
Nguzo dhidi ya Shurti
Iwapo mtu kasahau jambo fulani la shurti bila ya kuondoka mahali pake au
kituoni kwake, basi mtu atimize alichosahau, na hahitajiki kuleta sijida sahau.
Mtu akikumbuka shurti hiyo baada ya kutoka mahali pake au kituo chake
katika Swala, lakini kabla ya kufika nguzo nyingine, mtu arudie jambo hilo na
kulitimiza, kisha aendelee na Swala kuanzia hapo na kisha baada ya kutoa salam,
alete sijida sahau. (Kulifahamu jambo hili kunahitaji mtu ajue tofauti kati ya
vitendo na maneno ambayo ni nguzo za Swala na ajue zile ambazo ni shurti za
Swala).
Iwapo mtu anakumbuka kuwa kaacha shurti baada ya kufika katika nguzo
nyingine, basi shurti inaachiliwa mbali na mtu aendelee tu na Swala yake, alete
sijda sahau kabla ya kutoa salamu. Sababu ya Sijda sahau kuja hapa kabla ya
Salamu ni kwamba kuna jambo ambalo limeachwa na halikurudiwa. Hivyo, Sijida
sahau inachukua nafasi yake.
Hata hivyo, pale ambapo nguzo ya Swala inaachwa, mtu lazima arudi katika
nguzo hiyo na kuitimiza kwa sababu hiyo ndiyo inayoijenga Swala. Ndiyo kusema
kuwa swala huwa haiswihi bila nguzo hiyo. Kwa upande mwingine, shurti lazima
itimizwe, lakini inapotokea kuachwa bado Swala hubakia na nguzo zinazoijenga.
Hivyo Sijda sahau hufidia shurti iliyoachwa.
Aidha Swala hukamilika (hutimia) hata kama shurti imeachwa kwa makusudi.
Lakini kwa kufanya kusudi hiyo, yule anayeswali anakuwa ametenda dhambi.
Kwa mfano, kama mtu anainua kichwa chake juu kutoka kwenye sijida ya pili
katika rakaa ya pili ya al-asri, na anakaribia kusimama juu kwa ajili ya rakaa
ya tatu kisha akakumbuka kukaa kabla hajaanza kusimama wima sawasawa, basi hapo
mtu hahitajiki kuleta Sijida sahau.
Iwapo mtu kakumbuka kukaa kitako (katika jalsah) wakati akiwa katika
harakati za kusimama wima (wuquf), kabla hajanyoosha mgongo sawasawa, basi huyu
alete sijida sahahu baada ya kutoa salamu.
Kama mtu anakumbuka kuwa hakutoa shahada baada ya kuwa ameshainuka wima
kikamilifu, basi huyu asirudi kwenye shahada ya kwanza (ambayo ni shurti tu ya
swala na si nguzo), hiyo itaachwa tu katika swala hiyo, ila alete Sijida sahau
mwishoni mwa Swala kabla ya kutoa salamu.
Uthibitisho wa hilo ni Hadith ya Mtume, swallallahu alayhi wa sallam,
iliyosimuliwa na Bukhari na Muslim kwa mapokeo ya Abdullah ibn Buhaynah. Mtume,
swallallahu alayhi wa sallam, aliwaongoza Maswahaba wake katika Swala ya
Adhuhuri, akasimama wima baada ya rakaa ya pili (akiwa ameacha tashah-hud).
Basi Maswahaba nao wakainuka pamoja. Aliendelea na Swala hadi alipofikia
tashahudi (shahada) ya mwisho. Kisha akaleta Sijida sahau kabla ya kutoa
salamu.
Makosa ya Kuingiwa Shaka
1. Shaka ya kupuuzwa
‘Shakk’ ni neno la Kiarabu lenye maana ya hatihati ( “shaka”) juu ya lipi
kati ya mambo mawili limefanyika kweli. Katika Ibada, shaka hupuuzwa katika
hali hizi tatu:
1.
Pale kitu kinapokuwa sehemu ya hisia tu isiyo na msingi
wowote wa kweli kama vile mtu kujitilia shaka nafsini mwake
2.
Pale ambapo shaka katika Ibada inapokuwa jambo la kawaida kutokea kwa mtu kwamba ni
mara chache kwake kufanya tendo lolote la ibada bila kupata shaka. (Huu ni
mkakati mashuhuri wa Shetani wa kumfanya mtu achoke kumuabudu Mwenyezi Mungu.
3.
Pale shaka inapomjia mtu baada ya kumaliza ibada.
Iwapo, kwa mfano, mtu anaswali dhuhuri, anaikamilisha, na baada ya hapo
anaingiwa na shaka kama ameswali rakaa tatu au nne, basi mtu apuuzie shaka hii
isipokuwa kama atapata uhakika kuwa ameswali rakaa tatu (hasa pale mtu mwingine
aliyemwona atakapomwambia hivyo). Iwapo mtu kapata uhakika huo ndani ya dakika
chache baada ya Swala, basi akamilishe rakaa alizoacha, alete sijida sahau
baada ya Swala.
2. Shaka ya Kutiliwa Maanani
Pale mtu anapokuwa na shaka na jambo fulani ambalo
ni nguzo ya kufanya swala yake iswihi huku akiwa anaswali, basi hilo si jambo
la kupuuziwa. Ikiwa mtu anayeswali ana shaka juu ya kipi kati ya vitu viwili
kimetokea lakini ana uhakika zaidi na kimoja kuliko kingine, basi mtu aegemee
katika kile ambacho ana uhakika nacho zaidi na amalize Swala hivyo hivyo. Kisha
alete Sijida sahau baada ya kutoa salamu.
Kwa mfano, mtu anayeswali Swala ya al-asri, ana
shaka iwapo yupo katika rakaa ya pili au ya tatu, lakini anaelekea zaidi
kudhani kuwa yupo katika rakaa ya tatu, basi ajihesabu yupo katika rakaa hiyo
ya tatu, na aje kuleta sijda sahau baada ya kutoa salamu.
Uthibitisho wa hilo ni kauli ya Mtume, swallallahu
alayhi wa sallam, iliyosimuliwa na Bukhari na Muslim kwa mapokeo ya Abdullah
ibn Masoud. Mtume, swallallahu alayhi wa sallam, amesema, “Iwapo mmoja wenu ana
shaka katika Swala yake, basi ajaribu kulisia kile kilicho sahihi na amalize
swala yake kwa kuegemea (kile anacholisia ni sahihi zaidi), kisha atoe salamu,
halafu ndio alete sijda mbili (sijdasahau).”
Iwapo mtu anayeswali ana shaka juu ya lipi kati ya
mambo mawili ni sahihi na moja kati ya hayo mawili halina uhakika sana kichwani
mwake kama lile jingine, basi aigemeze Swala yake katika lile analoona lina
uhakika hata kama ni kidogo sana-na kisha alete sijida sahau kabla ya kutoa
salamu
Kwa mfano, kama mtu anaswali swala ya al-asri na
ana shaka iwapo yupo katika rakaa ya pili au ya tatu, na hakuna moja kati hayo
mawili lenye uhakika zaidi kuliko jingine, basi hapo ajihesabu kuwa yupo katika
rakaa ya pili na aje kuleta sijida sahau baada ya shahada (tashah-hud) lakini
kabla ya kutoa salamu.
Uthibitisho wa hili ni Hadith ya Mtume,
swallallahu alayhi wa sallam, iliyopokelewa kutoka kwa Abu Said al-Khudhri.
Mtume, swallallahu alayhi wa sallam, amesema, “Iwapo mmoja wenu anapata shaka
katika Swala yake kama ile ya kutojua rakaa ngapi ameshaswali, iwe tatu au nne,
basi aondoshe shaka na aegemeze swala yake katika lile alilo na uhakika nalo,
baadae alete sijida mbili kabla ya kutoa salamu. Hivyo, kama ameswali rakaa
tano, basi (sijida hizi) huishufaia Swala yake. Na kama kaswali rakaa nne, basi
(sijida hizi) huitangulia hila ya Shetani” (ya kumvuruga au kumuharibia Swala).
Moja ya hali ambazo kwazo shaka, kwa kawaida,
huzuka ni pale mtu anapounga Swala wakati Imamu yupo katika rukuu ambapo
mchelewaji hana uhakika kama ameuwahi muda wa kuhesabiwa kuwa kaipata rukuu au
la. Ikiwa mchelewaji anaona moja lina uwezekano mkubwa zaidi (kati ya ama
kaiwahi rukuu au kaikosa), basi aiegemeze Swala yake katika lile analoona lina
uwezekano zaidi. Kisha baada ya kutoa salamu ndipo alete sijidasahau.
Iwapo Mswaliji anaunga swala katika hali hiyo,
huku Imamu akiwa katika rakaa ya kwanza, na mchelewaji akawa na uhakika mkubwa
kuwa kaiwahi rukuu katika muda wake, basi Swala yake inajuzuishwa kwamba
hakukosa jambo lolote katika Swala hiyo, na kwa hali hiyo, asilete sijidasahau.
Lakini kama hakuna uwezekano unaouzidi uwezekano
mwingine, yaani shaka iko sawa kwa sawa katika mambo mawili, basi aegemeze
Swala yake katika lile linaloweza kukatiwa hukumu kuwa ndilo la hakika
zaidi-nalo ni kwamba mtu ana hakika kuwa kaunga swala lakini huenda ameikosa
rukuu ya kwanza jambo ambalo lina maana kuwa kaikosa rakaa ya kwanza.
Hivyo, kwa vile hana uhakika na rakaa ya kwanza,
basi aihesabu kuwa kaikosa. Baada ya Imamu kutoa salamu, ailipe rakaa hiyo,
kisha alete sijida sahau kabla ya kutoa salaam.
Iwapo mtu anayeswali ana shaka iwapo kweli
katimiza jambo fulani katika Swala yake au la, basi aegemeze Swala yake katika
lile analoona lina uwezekano mkubwa zaidi (ambalo ana uhakika nalo zaidi kuwa
limetokea), lakini baadae akatanabahi kuwa kumbe lile alilolipa uwezekano mdogo
ndilo hasa lililotokea, basi kwa mujibu wa Maulamaa kadhaa, halazimiki kuleta
sijidasahau kwa sababu ile sababu ya kufanya hivyo, yaani shaka,
imeshaondoshwa.
Wengine rai yao ni kwamba bado mtu huyo
anawajibika kuleta sijidasahau ili kumtangulia Shetani kufuatana na kile
alichosema Mtume, swallallahu alayhi wa sallam, katika Hadith
iliyokwishanukuliwa hapo juu. “Basi (sijida) hizo mbili huitangulia hila ya
Shetani.” Mbali ya hivyo, hapo mtu huiswali sehemu ya Swala yake katika hali ya
shaka. Ndiyo kusema, ulazima wa kuleta sijidasahau unabaki palepale. Rai hii ya
pili ndiyo yenye uhakika zaidi.
Mathalani, mtu anayeswali anaingiwa na shaka juu
ya iwapo yupo katika rakaa ya pili au ya tatu, na hakuna uwezekano unaouzidi
mwingine. Kwa hiyo, hapo mtu atajihesabu kuwa yupo katika rakaa ya pili, lakini
punde akatanabahi kuwa, kweli yupo katika rakaa hiyo ya pili. Katika hali hii,
rai iliyopendelewa ni kwamba bado mtu huyo alete sijidasahau ambapo nafasi
sahihi ya sijida hiyo ni kabla ya kutoa salamu.
Sijida-Sahau Unaposwali Nyuma ya Imamu
Iwapo Imamu anafanya kosa na kisha kuleta sijidasahau, wale walio nyuma
yake katika Swala wanawajibika kumfuata vyovyote atakavyoileta sijida hiyo, ama
afanye hivyo kabla au baada ya kutoa salamu. Tofauti pekee ni iwapo Imamu
anatoa salamu kabla ya kuleta sijida sahau huku mtu akiwa ameikosa sehemu ya
swala hiyo.
Katika hali hiyo, pale Imamu anapotoa salamu, mchelewaji atasimama juu
kukamilisha kile ambacho amekikosa. Kisha atatoa salamu, halafu ataleta sijida
sahau, kisha atatoa tena salamu. Katika mazingira haya, yeye anakuwa na udhuru
wa kuacha kuleta sijidasahau pamoja na Imamu kwa sababu makatazo ya kumaliza
Swala kabla ya kufika mwisho wake ndiyo yenye nguvu zaidi.
Uthibitisho wa hili ni kauli ya Mtume, swallallahu alayhi wa sallam,
iliyosimuliwa na Bukhari na Muslim kwa mapokeo ya Abu Hurayrah: “Kwa hakika,
Imamu hayupo kwa ajili ya kingine ila kufuatwa, Kisha msiachane naye...Na
anapoleta sijidasahau basi nanyi fanyeni hivyo (leteni sijida hiyo).”
Ikiwa mtu anayeswalishwa kafanya kosa lake mwenyewe, maadam hakukosa sehemu
yoyote ya Swala hiyo, basi huyu haleti sijidasahau, kwani akifanya hivyo,
atakuwa anaachana na Imamu.
Lakini mtu anayeswalishwa anapoghafilika na kukosa sehemu ya Swala, au
akifanya kosa wakati akiwa analipa chochote alichokikosa katika Swala, basi
huyu lazima alete sijidasahau mwishoni mwa Swala ama kabla au baada ya kutoa
salamu (tasliim), kutegemeana na kosa kama ilivyokwishafafanuliwa huko nyuma.
Kwa mfano, iwapo mtu anayeswalishwa (maamuma) kasahau kusema “subhana rabbi
al-adhiim” ambayo ni shurti katika rukuu, lakini mtu huyu hakuacha nguzo za
swala akiwa na Imamu, basi huyu haleti sijidasahau.
Huu ni mfano mwingine: Tuseme mtu kaghafilika wakati akiswali dhuhuri nyuma
ya Imamu, na akadhani rakaa ya tatu ni ya nne. Imamu akasema
Allahu Akbar na kuinuka kutoka kwenye sijida kusimama juu, huku yule
maamuma aliyepitiwa akitoka kwenye sijida na kukaa kitako (jalsa). Pale
anapotambua kosa lake na kuungana tena na Imamu kabla ya kukosa rakaa ya nne,
basi huyu haleti sijida sahau.
Hata hivyo, katika hali isiyo na uwezekana mkubwa
sana wa kutokea, kama maamuma huyo atabaki amekaa na kuikosa rakaa ya nne
kutokana na mghafala na mkanganyiko, basi baada ya Imamu kutoa salamu, maamuma
huyu aliyeghafilika atalazimika kulipa sehemu aliyoikosa, kisha atatoa salamu,
halafu ataleta sijidasahau ili kufidia kosa la kuongeza kikao (jalsa) katika
Swala hiyo.
Sasa basi, ikiwa mtu aliye katika Swala atafanya
kosa zaidi ya moja, bado alete sijidasahau ileile moja. Na iwapo katika makosa
mawili, moja linahitaji kuleta sijidasahau kabla ya kutoa salamu ya kumaliza
Swala, na jingine linahitaji sijida sahau baada ya kutoa salamu, basi alete sijidasahau
kabla ya salamu tu basi.
Kwa mfano, tujaalie mtu kaikosea rakaa yake ya
pili na (kuifanya) kuwa ya kwanza. Baada ya hapo anasimama wima kwa ajili ya
rakaa ya tatu, huku yeye akidhani ni ya pili, hivyo akasimama bila kuleta
tashah-hud (shahada) ya kikao cha kwanza. Kisha baada ya rakaa ya tatu, yeye
ndio analeta tashah-hud ya kwanza, lakini punde anatambua kosa lake. Kwa maneno
mengine, aliiacha shahada ya kwanza jambo ambalo linalazimu kuleta sijidasahau
kabla ya kutoa salamu-na akaongeza tashah-hud baada ya rakaa ya tatu jambo
ambalo linahitaji sijidasahau baada ya kutoa salamu.Katika hali hii, analeta
sijida sahau ile ile moja kabla ya kutoa salamu.
Ijue Tofauti kati ya
Nguzo na Sunna katika Swala
Nguzo zina maana ya kile kinachofahamika kama arkan (rukn) katika Lugha ya
Kiarabu, hivi ni vipengele vya Swala ambavyo vinaaminika kuwa ni vya msingi mno
kiasi ambacho kuacha chochote kati ya hivyo kutaibatilisha Swala nzima.
Vipengele vingine vya Swala vimedarajishwa kulingana na umuhimu wao kama
ilivyobainishwa katika Sunna. Vinavyofuata kwa uzito kulingana na Sijda sahau
ni vile vipengele ambavyo, vinapoachwa hutakiwa kurudiwa lakini huhitaji sijida
sahau-zinazoitwa Sunna kwa mujibu wa Maulamaa wa Hanafi, Maliki, na Shafi’i na
ni Wajibu kwa mujibu wa madh-hab ya Hanbal. Ni jambo muhimu kwamba mtu atambue
kwamba Madh-hab mbalimbali za Fiqh zinatofautiana kidogo sana katika
kuviainisha vipengele hivyo. Iliyoorodheshwa hapa chini ni mifano ya arkan
(nguzo) na Sunna kwa mujibu wa Madh-hab ya Shafii ambayo ndiyo yanayoainisha
idadi kubwa ya nguzo (arkan). Madh-hab
ya Malik na Hanbal yanaainisha vipengele 14 vya Swala kama nguzo (arkan) wakati
ambapo Madh-hab ya Hanafi yanaonesha nguzo Sita tu.
Nguzo 17 za Swala
1.
Nia
2. Kuhirimia “Allahu Akbar”
3. Kusimama
4. Kusoma Al-Fatiha
(Alhamdu)
5. Kurukuu
6. Kutulia bila kutikisika
katika rukuu
7. Kuitidali (kuinuka na
kunyooka mgongo baada ya kurukuu)
8. Kutulia katika itidali
9. Kupomoka hadi kusujudu
chini
10.
Kutulia katika
Sijda
11.
Kukaa kikao (baada ya kutoka sijidani)
12.
Kutulia katika
kikao hicho
13.
Kutoa shahada
14.
Kukaa katika shahada
15.
Kumswalia Mtume
baada ya kutamka shahada
16.
Kutoa salamu
17.
Kuzifuata Nguzo hizo kwa mlolongo wake sahihi
Sunna Kuu Sita za Swala
(Zinapoachwa, huhitaji kuletwa Sijda
Sahau)
1.
Tashahudi ya kwanza ya Swala (shahada inayotolewa katika
kikao cha kwanza cha Swala)
2.
Kukaa wakati wa kutoa shahada hiyo
3.
Kumswalia Mtume baada ya shahada hii
4.
Kuwatakia rehema ahali zake
5.
Kuleta Dua (Qunut) baada ya rukuu ya pili ya swala ya
Alfajiri
6.
Kusimama wima katika dua hiyo.
v Imeandaliwa na
Na Omar Haliim, Mfasiri S. Hussein
Edited and posted by
Yusouf hassan sanga
Jazakallah khairan na Allah awazidishie ujuzi ili muweze kutunufaisha zaidi ndugu zenu katika imani.
ReplyDelete