Sala ya Ijumaa
Imeitwa Sala ya Ijumaa kwa vile inasaliwa siku ya Ijumaa,
au kwa yale ya kheri yaliomo kwenye siku hii. Sala ya Ijumaa ni bora yao ya
Sala na siku ya Ijumaa ni bora yao ya siku. Hivi ni kwa qauli ya Mtume s.a.w.:
"Bora ya siku zilizochomoza jua juu yake ni siku ya
Ijumaa, siku hio ameumbwa Adam a.s., na siku hio ametiwa Peponi, na siku hio
ametoka Peponi, wala hakitasimama Qiyama isipokuwa siku ya Ijumaa".
(Imehadithiwa na Muslim na Abu Daud na Al Nissaai na Al Tirmidhy).
Hukmu Yake
Sala ya Ijumaa ni waajibu kwa Qauli ya Mwenyezi Mungu
Mtukufu, qauli ya Mtume s.a.w. na itifaqi ya wanazuoni. Ametwambia Mwenyezi
Mungu Mtukufu:
"Enyi mlio amini! Ikiadhiniwa Sala siku ya Ijumaa, nendeni
upesi kwenye dhikri ya Mwenyezi Mungu, na wacheni biashara ……". (Al Jumu'a
: 9).
Na amesema Mtume s.a.w.:
"Niliazimia nimuamrishe mtu asalishe, kisha nende
nikawachomee moto nyumba zao watu wasiokwenda kusali Sala ya Ijumaa ".
(Imehadithiwa na Muslim).
Na katika upokezi mwengine:
"Wasiwache watu kutekeleza Sala ya Ijumaa, wakiwacha
Mwenyezi Mungu atapiga mihuri kwenye nyoyo zao na hapo watakuwa miongoni mwa
walioghafilika". (Imehadithiwa na Muslim na wengineo).
Na Hadithi nyengine ya Matume s.a.w.: "Kuiendea Sala
ya Ijumaa ni waajibu kwa kila balegh". (Imehadithiwa na Al Nissaai).
Na Hadithi nyengine ya Mtume s.a.w.:
"Mwenye kuwacha kusali Sala ya Ijumaa,
Ijumaa tatu (mfululizo); Mwenyezi Mungu hupiga muhuri kwenye moyo wake".
(Imehadithiwa na Abu Daud na Al Tirmidhy na Al Nissaai).
Shuruti za Kuwajibikia Sala ya Ijumaa
Shuruti za kuwajibikia Sala ya Ijumaa ni saba:
Ya Kwanza, Uislam, kama ilivyotajwa kwenye Kitabu cha Sala.
Ya Pili mpaka ya Sita, kuwa huru, baalegh, mwenye akili kamilifu, mwanamume, mzima
wa siha. Hivi ni kwa qauli ya Mtume
s.a.w.:
"Sala ya Ijumaa ni waajibu kwa kila Muislam, isipokua
kwa watu wanne, mwenye kumilikiwa, mwanamke, mtoto mdogo na mgonjwa".
(Imehadithiwa na Abu Daud).
Mgonjwa wa akili yeye si mwenye kukalifishwa na Sharia kwa
lolote lile. Kwenye hukmu ya ugonjwa imekisiwa kuingia, kukosa cha kusitiri
utupu, kukhofu dhulma na madhaalim, na mwenye tumbo la kuendesha na hawezi
kujizuia; lau itakhofiwa maiti kuharibika, watu wataacha kwenda
kusali Sala ya Ijumaa na kumshughulikia maiti mpaka
kumzika.
Ya Saba, mkaazi, si msafiri; haimuwajibikii Sala ya Ijumaa msafiri.
Hivi ni kwa vile haikupokewa kuwa Mtume s.a.w. amewahi kusali Sala ya Ijumaa
nae yumo safarini, bali imepokewa kuwa: "Haimlazimu Sala ya Ijumaa aliomo
safarini". (Imehadithiwa na Al Bayhaqy).
Shuruti za Kusihi Sala ya Ijumaa
Mbali na shuruti za Sala tulizotangulia kuzitaja, kusihi
Sala ya Ijumaa ina shuruti tatu ziada:
Ya Kwanza, iwe kwenye pahala wanapoishi idadi ya watu wenye kutimiza
Sala ya jama'a, kwa aina yoyote ile ya majengo.
Ya Pili, isaliwe jama'a; haikuwahi kupokewa kwamba Mtume wetu Mpezni
s.a.w. au Makhalifa wa baada yake wamewahi kusali Sala ya Ijumaa mtu peke yake.
Idadi ya watu wenye kufanya jama'a ya kulazim Sala ya Ijumaa wasipungue watu
arubaini. Kwa Hadithi ya Jaabir r.a. kwamba:
"Imekuwa
ni mwenendo kwamba kila penye watu arubaini na zaidi (husaliwa) Sala ya
Ijumaa". Imehadithiwa na Al Bayhaqy).
Na kwa Hadithi ya Ka'ab bin Malik r.a.:
"Mtu wa mwanzo
kutusalisha Sala ya Ijumaa kwenye kijiji cha Khudhamaat ni As'ad bin Zaraara na
tulikuwa watu arubaini". (Ibnu Hibbaan na Al Bayhaqy waimeipa darja ya
Hadithi sahih).
Na kwa Hadithi nyengine kwamba Mtume s.a.w.:
"Mtume s.a.w. amesali Sala ya Ijumaa
akiweko Madina, wala haikupokewa kutoka kwake kwamba alisali Sala ya Ijumaa kwa
uchache ya watu arubaini".
Ya Tatu, isaliwe kwenye wakati wake, wakati wake ni ule wakati wa
Sala ya adhuhuri. Hivi ni kwa qauli ya Anas r.a.:
"Mtume s.a.w. alikuwa akisali Sala ya
Ijumaa baada ya kutenguka jua". (Imehadithiwa na Al Bukhary).
Imepokewa kutoka kwa Salama bin Al Aku'i r.a.:
"Tulikuwa tukisali Sala ya Ijumaa pamoja
na Mtume s.a.w. linapotenguka jua".
Ikiwa itakuwa dhiki ya wakati, ikawa haiwezekani kusaliwa
Sala ya Ijumaa, basi itasaliwa Sala ya adhuhuri badala ya Sala ya Ijumaa. Ikiwa
wataingiwa na shaka kama wakati umetoka au laa, basi watasali Sala ya adhuhuri,
kwani kuhakikisha kuweko wakati ni sharti ya kusihi Sala.
Fardhi za Sala ya Ijumaa
Fardhi za Sala ya Ijumaa ni tatu:
Ya Kwanza, itanguliwe na khutba mbili, baina ya khutba na khutba
kitako. Imepokewa kutoka kwa Jaabir bin Samra r.a. kwamba Mtume s.a.w.:
"Mtume s.a.w. alikuwa akikhutubu khutba
mbili na akikaa baina ya khutba mbili hizo, na akikhutubu hali amesimama".
Imepokewa vile vile:
"Hakika ya Mtume s.a.w. alikuwa
akikhutubu khutba mbili, akisoma Qur'ani na akiwaadhi watu".
Nguzo za Khutba ya Ijumaa
Khutba ya Sala ya Ijumaa ina nguzo tano:
Kwanza, kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu.
Pili, kumsalia
na kumuombea Rehma Mtume s.a.w.
Tatu, kuusia
watu kumcha Mwenyezi Mungu Mtukufu.
Nne, kuwaombea
du'a Waumini kwenye khutba ya pili.
Tano, kusoma
Qur'ani; uchache wake ni Aya kaamili.
Shuruti za Khutba ya Sala ya Ijumaa
Khutba ya Sala ya Ijumaa ina shuruti saba:
Kwanza, kuingia wakati wa Sala.
Pili, kutangulia
khutba mbili kabla ya Sala.
Tatu, kusimama;
kwa mwenye kuweza.
Nne, kukaa
kitako baina ya khutba mbili kwa kiasi cha kutulia.
Tano, ku'tahirika
na hadathi kubwa na ndogo na najsi (uchafu), mwilini, nguoni, na mahala
pakusalia.
Sita, kusitiri
utupu kwa nguo ilio 'taahir.
Saba, kutoa
sauti ya kusikilika na watu arubaini ambao wanalazimika na hii Sala.
Fardhi ya Pili, isaliwe raka'a mbili; hivi ni kwa qauli ya Sayyidna 'Umar
r.a.:
Maana yake ni kama hivi: "Sala ya Ijumaa ni raka'a
mbili bila ya kupunguza, kama alivyosema Mtume s.a.w.".
Fardhi ya Tatu, isaliwe jama'a; tumeshataja dalili ya hivi.
Haiati (Mapambo) ya Sala ya Ijumaa
Inasuniwa kwa mwenye kwenda kusali Sala ya Ijumaa, mambo
manne:
La Kwanza, akoge, hivi ni kwa qauli ya Mtume s.a.w.:
"Mwenye kwenda kusali Sala ya Ijumaa basi
naakoge". (Imehadithiwa na Al Sheikhan).
La Pili, asafishe kiwiliwili chake uchafu wenye kusababisha harufu
mbovu ya mwili, na hivyo ndivyo inavyokusudiwa kwa kusemwa akoge, sio basi
ajimwagie maji. Amesema Imam Shafi'ii r.a.:
"Mwenye kunadhifisha nguo zake hupungua wasiwasi wake,
na mwenye kufanya harufu yake kuwa nzuri (kujitia manukato) huzidi akili
yake".
La Tatu, kujipamba kwa kuvaa nguo nzuri na kwa kujitia manukato.
Hivi ni kwa qauli yake Mtume s.a.w.:
"Mwenye kukoga siku ya Ijumaa na akavaa nzuri mno ya
nguo zake na akajitia manukato kutoka nyumbani kwake - ikiwa anayo - kisha
akenda kusali Ijumaa, akiingia msikitini asikiuke watu waliokwishakaa (kutaka
kwenda mbele), kisha akasali alicho andikiwa, kisha akamsikiliza imam, mpaka
akamaliza Sala yake; huwa ni kafara kwake kwa kiliopo baina ya Ijumaa hii na
Ijumaa iliopita". (Imepokewa na Ibnu
Hibban na Al Haakim).
Kuvaa nguo nyeupe kwa kuhudhuria Sala ya Ijumaa ni bora
zaidi. Hivi kwa qauli ya Mtume s.a.w.:
"Vaeni nguo nyeupe, kwani hizo ni bora
mno ya nguo zenu; na kwa nguo nyeupe wakafinini maiti wenu".
La Nne, kukata kucha na nywele zenye kupendeza kuondolewa; kwani
hivi ni katika unadhifu.
Kusikiliza Khutba na Khilafu Ziliopo
Wamekhitalifiana rai wanazuoni juu ya hukmu ya kuzungumza
wakati wa khutba ya Sala ya Ijumaa. Amesema Imam Shafi'ii r.a. na Imam Malik na
Imam Abu Hanifa r.a. na Imam Ahmad r.a. kwamba inaharimishwa kuzungumza wakati
wa khutba ya Sala ya Ijumaa. Wao wametolea hoja Qauli ya Mwenyezi Mungu
Mtukufu:
"Na isomwapo Qur'ani isikilizeni na mnyamaze ili
mupate kurehemiwa". (Al
Aáraaf: 204).
Wamesema wengi wa wafasiri wa Qur'ani kwamba Aya hii
imeteremshwa kukhusu khutba ya Sala ya Ijumaa. Na imeitwa hii khutba kwa jina
la Qur'ani kwa vile imo ndani yake Qur'ani Tukufu. Na qauli ya Mtume s.a.w.:
" Ukisema
kumwambia sahibu yako kwenye Sala ya Ijumaa na Imam anakhutubu - sikiliza -
basi itakuwa umefanya kosa". (Imehadithiwa na wapokezi wa Hadithi
isipokuwa Ibni Maajah).
Na rai nyengine ya Imam Shafi'ii r.a. ni kwamba
haiharimishwi kusema, bali kusikiliza ni sunna kama walivyopokea Al Sheikhan
kuwa Sayyidna 'Uthman r.a aliingia msikitini siku ya Ijumaa na Sayyidna 'Umar
r.a. anakhutubia, akasema Sayyidna 'Umar r.a. kumwambia Sayyidna 'Uthman r.a.:
"Nini hali ya watu wanataakhari kuitikia wito?” Akasema Sayyidna 'Uthaman
r.a.: “Yaa Amir-l-Muuminiin! Baada ya kusikia adhana, nimetia udhu na nikaja
msikitini". Na imehadithiwa kuwa wakati Mtume s.a.w. yuko juu ya membari
anakhutubia siku ya Ijumaa aliingia mtu na kuuliza kwa kelele: "Lini
Qiyama"? Watu wakamuashiria anyamaze, lakini hakufanya hivyo. Na akarejea
na maneno yake, baada ya dakika Mtume s.a.w. akasema kumwambia: "Na uwe
pole, umekiandalia nini?” Akasema yule mtu: "Mapenzi ya Mwenyezi Mungu na
Mtume wake". Akasema s.a.w.: "Hakika yako wewe na unaempenda". (
Imehadithiwa na Al Bayhaqy ).
Hoja ya kwamba kusema wakati wa khutba si haraam ni vile
kuwa Sayyidna 'Uthman r.a. alisema kwa kumjibu Sayyidna 'Umar r.a., na kwamba
Mtume s.a.w. hakumkanya yule alieuliza lini Qiyama, na lau kama ni haraam basi
angalimkanya kusema. Hii khilafu iliopo kukhusu kusema au kutosema haikhusiani
na kitu muhim na cha dharura, katika hali hio haikatazwi kusema; bali ni
waajibu kusema; kama vile kumuongoza kipofu, au kuona mtu anatambaliwa na nnge
ukamzindua, au kumuona dhaalim amemuandama mtu ukamtanabahisha, au kuamrisha
mema na kukataza maovu.
Kujuzu Kusali wakati Imam Anakhutubu
Wamekhitalifiana rai wanazuoni juu ya kwamba mtu akiingia
msikitini siku ya Ijumaa na Imam anakhutubu, inajuzu asali raka'a mbili za
tahiyatu-l-masjid au asisali. Wamesema baadhi ya wanazuoni kuwa asisali, na
imepokewa hivi kutoka kwa Ibni 'Umar r.a., na Sayyidna 'Uthman r.a. na Sayyidna
'Ali r.a.; na kwa hii amri ya kusikiliza. Wakatoa dalili juu ya kisa cha Saliik
r.a. kwamba alikuwa hana nguo, Mtume
s.a.w. akamuamrisha asimame ili watu wamuone wampe sadaqa. Amesema Imam
Shafi'ii r.a. na Ahmad na Is-haaq na wanazuoni wakisasa wengine kuwa
inapendekezwa asali tahiyatu-lmasjid raka'a mbili fupi kabla ya kukaa, wao
wametolea hoja hivi kwa qauli ya Mtume s.a.w. juu ya Saliik wakati alipoingia
msikitini akakaa kitako na Mtume s.a.w. anakhutubia kwenye Sala ya Ijumaa,
Mtume s.a.w. alimuuliza Saliik: "Umesali ewe fulani?” Akajibu:
"Laa", yaani si kusali; Mtume
s.a.w. akamwambia: , yaani inuka uruku'i, yaani
usali. Na katika upokezi mwengine: yaani inuka usali raka'a mbili. Na katika
upokezi mwengine: yaani sali raka'a mbili. Na katika upokezi
mwengine:
"Akiingia mmoja wenu msikitini siku ya
Ijumaa na Imam anakhutubu, basi naasali raka'a mbili". Na katika upokezi
mwengine:
"" "……., na Imam anakhutubia, naaruku'i
raka'a mbili, na azifupishe".
Hadithi zote hizi zimo kwenye Kitabu cha Hadithi cha Imam
Muslim r.a. na zimetaja wazi kupendeza kusali raka'a mbili khafifu za (kuamkia msikiti) unapoingia msikitini siku ya Ijumaa na
Imam anakhutubu. Hivi ni kwa mwenye kuingia msikitini na Imam ana khutubu. Ama
yule aliyomo msikitini tangu kabla ya Imam kuanza khutba, na akainuka kusali
wakati Imam anakhutubu, hivi haijuzu; hata ikiwa kwa raka'a khafifu.
Kusoma Surat Al-Kahfi
Inasuniwa kusoma Surat Al-Kahfi, usiku wa kuamkia Ijumaa
(Alkhamis usiku kuamkia Ijumaa), au Ijumaa yenyewe. Kusoma Surat Al-Kahfi
mchana wa Ijumaa kumekuja kwa qauli ya Mtume s.a.w:
"Mwenye kusoma Surat
Al-Kahfi siku ya Ijumaa hun'garishiwa nuru baina ya Ijumaa na Ijumaa".
(Imehadithiwa na Al Haakim na Al Bayhaqy).
Kusoma Surat Al-Kahfi usiku wa kuamkia Ijumaa kumekuja kwa
qauli ya Mtume s.a.w:
"Mwenye kuisoma (yaani Surat Al-Kahfi) usiku wa
kuamkia Ijumaa hun'garishiwa nuru (yenye kuenea) baina yake na baina ya
Bait-l-'atiiq (Msikiti wa Makka)". (Imehadithiwa na Al Bayhaqy).
Ni waajibu mtu anaposoma Qur'ani - Surat Al-Kahfi - au Sura
nyengine yoyote ile, iwe si kwa kumghasi au kumshawishi mwenzake anaesoma, au
anaesali au mwenye kuvuta uradi; kwa vile yeye kusoma kwa sauti ya kughasi.
Kufanya hivyo ni haraam, amesema Mtume
s.a.w. :
"Hakika kila mmoja wenu ni mwenye kusema na Mola wake
Mlezi, basi musiudhiane, walaa asitoe sauti mmoja wenu wakati akisoma".
Wakati bora wa kusoma Surat Al-Kahfi ni baada ya Sala ya alfajiri, kwa
kukimbilia kheri. Ama vile wanavyofanya watu wengi, yaani kuisoma msikitini na
kwa sauti ya kughasi wengine katika ibada zao, hivi haifai; bali imeharimishwa.
Saa ya Kutakabaliwa Du'a
Imesuniwa kuzidisha du'a usiku wa kuamkia Ijumaa na mchana
wake, kuzidisha du'a mchana wa Ijumaa kwa kutumaini Inshaallah isadifu du'a
yake saa ya kutakabaliwa du'a . Amebainisha Mtume s.a.w. Saa
ya Ijaaba “saa ya kutakabaliwa du'a” kwa kutufunza:
"saa
ya kutakabaliwa du'a", ni baina ya Imam anapokaa kitako cha baina ya
khutba mbili na mpaka kumalizika Sala".
Ameeleza Imam Shafi'ii r.a. kwamba du'a yenye kupendeza
zaidi kusomwa usiku wa kuamkia Ijumaa ni kumsalia Mtume s.a.w.
Kumsalia Mtume s.a.w.
Inasuniwa kumsalia Mtume s.a.w. usiku wa kuamkia Ijumaa na
mchana wake, hivi ni kutokana na qauli yake s.a.w.:
"Hakika bora mno ya siku zenu ni siku ya Ijumaa, basi
kithirini kunisalia siku hii; kwani ninaoneshwa sala zenu ". Na amesema
Mtume s.a.w.:
"Fanyeni mno kunisalia
usiku wa kuamkia Ijumaa na mchana wake, kwani mwenye kunisalia mara moja
Mwenyezi Mungu Mtukufu humsalia yeye mara kumi".
Kuharamishwa Biashara Baada ya Adhana
Imeharimishwa baada ya adhana ya Sala ya Ijumaa kufanya
biashara na ya mfano wake. Hivi ni kwa Qauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:
"Enyi mlio amini! Ikiadhiniwa
Sala siku ya Ijumaa, nendeni upesi kwenye dhikri ya Mwenyezi Mungu, na wacheni
biashara, ……". (Al Jumu’a : 9).
Kuharamishwa biashara kumeingia na kila la mfano wake ambalo
litaachisha kukimbilia kwenda kusali. Pia ni makrouh kujishughulisha na mambo
ambayo si ya kwendea kwenye Sala baada ya kuingia wakati wa Sala, yaani baada
ya jua kutenguka; kabla ya adhana. Ama baada ya adhana ni haraam.
Sala za Idi Mbili
Neno 'Idi, linatokana na neno , yaani kurejea kila mwaka;
au inarejea furaha kwa kurejea idi, na wingi wa ne'ema za Mwenyezi Mungu
Mtukufu kwa viumbe vyake. Sala ya Idi imekuja kwa Qauli ya Mwenyezi Mungu
Mtukufu, na kwa Hadithi za Mtume s.a.w. na kukubaliana wanazuoni. Amesema
Mwenyezi Mungu Mtukufu:
"Basi Sali na uchinje kwa ajili ya Mola wako
Mlezi". (Al Kawthar : 2 ).
Hii Sala iliotajwa hapa ni hii Sala ya Idi Al Adh-ha (Idi
ya siku ya kuchinja). Mtume s.a.w. alikuwa akisali yeye na Masahaba zake Sala
za Idi mbili, Idi ndogo, Idi-l-fi'tri; ya baada Ramadhani na Idi kubwa,
Idi-l-Adh-ha, Idi ya kuchinja, (idi ya mfunguo tatu). Idi ya mwanzo aliosali
Mtume s.a.w. ni Idi ya baada Ramadhani katika mwaka wa pili wa Hijria, na
katika mwaka huu ndio ikafaradhishwa Zakatu-l-fitri, Zaka inayotolewa kwa
kumaliza saumu ya Ramadhani.
Sala ya Idi ni "sunna iliotiliwa nguvu", hivi
ni kwa qauli ya Mtume s.a.w. alipomjibu Bedui alieuliza kama analazimika na
Sala nyengine baada ya Sala tano: "Je, nina lazimika na nyengine"? Akasema
s.a.w.: "Laa, ila ikiwa ni sunna". (Imehadithiwa na Al Sheikhan).
Na inasemwa kuwa ni .
Fardhi kifaya, ni fardha ambayo wakifanya baadhi ya watu huanguka waajibu kwa
wote, na isipofanywa na yeyote huwa dhambi kwa wote; kama vile kumshughulikia
maiti mpaka kumzika. Wamesema wanazuoni kuwa Sala ya Idi ndogo na Idi kubwa ni
fardhi kifaya, wakiwacha watu kusali watapata 'iqabu wote, hivi ni kwa vile
hizi Sala ni amri ya Mwenyezi Mungu Mtukufu na ni mwenendo wa Mtume s.a.w. na
ni miongoni mwa alama za umoja wa Waislam.
Sala ya Idi husaliwa jama'a, bali pia inajuzu mtu kusali
peke yake. Mwanamke nae anaruhusiwa kusali Sala ya Idi jama'a, lakini vijana wa
kike inakatazwa kwao wao kuhudhuria Sala ya Idi jama'a, kwa kuepuka fitna; kwa
vile aghalabu yao ni wenye maumbo ya kuvutia. Hivi ni kwa vile kuharimishwa kwa
vijana wa kike na wanawake wenye umbo zuri la kuvutia - japo wakiwa wakubwa wa
umri - kujitoa nje; hivi ni hadhar ya kuepusha fitna katika hali na zama hizi
zilizozidi njia na hali za ufisadi.
Na Hadithi ya Umu 'A'tiyah r.a., na ikiwa ina maanisha
kujuzu kwenda kusali Sala ya Idi, lakini namna ya hali iliokuwepo wakati ule wa
karne za kheri ishaondoka; nayo ni uchache wa Waislam, hivyo ndio akaruhusu
Mtume s.a.w. wanawake wende kwenye Sala ya Idi ili uongezeke wingi wa Waislam
kwenye Sala ya Idi, na kwa ajili hii ndio s.a.w. akaruhusu hata waliomo kwenye
hedhi - siku zao - kuhudhuria Sala ya Idi, hali ya kuwa wao hawana kusali. Na
vile vile zama hizo zilikuwa zama za amani, wanawake walikuwa hawajitoi na
mapambo na kuonesha maumbo yao, na walikuwa ni wenye haya, walikuwa macho
chini, hali kadhaalika wanaume. Ama zama zetu za leo, ni hakika ya kutokea
fitna wakienda wanawake kusali jamaa. Kutokana na haya, ni ndivyo alivyosema
Sayyidah 'Aisha - Mama wa Waumini r.a. kwamba:
"Lau angaliona Mtume s.a.w. waliyoyazuwa wanawake
angaliwazuilia (kwenda) misikitini kama walivyozuiliwa wanawake wa Bani
Israili". Hii ndio fatwa ya Mama wa Waumini, Sayyidah 'Aisha r.a. ambayo
aliisema katika wakati wa kheri, na watu wengi (wanazuoni) wameichukulia hoja
qauli hii; miongoni mwao ni 'Arwa, na Al Qasim, na Yahya Al Ansari, na Malik,
na Abu Hanifa, (yeye mara akienda na qauli hii ya Sayyidah 'Aisha r.a. na mara
nyengine akijuzisha wanawake kwenda kusali Sala ya idi), na Abu Yusuf -
Mwenyezi Mungu Mtukufu awe radhi juu yao jami'i - Amin.
Wakati wa Sala za Idi
Wakati wa Sala za Idi ni tangu kuchomoza jua mpaka
kutenguka, lakini imesuniwa kuakhirisha kuisali mpaka jua liwe juu kiasi cha
urefu wa mkuki kama alivyofanya Mtume s.a.w., pia ili kuepukana na khilafu kwa
wenye kusema kuwa hauingii wakati wa Sala ya Idi mpaka jua lichomoze na kua juu
urefu wa mkuki. Imesuniwa kuisali mapema Sala ya Idi kubwa - Idi Adh-ha - na
kuichelewesha Sala ya Idi ndogo - Idi Alfi'tri. Amehadithia Imam Shafi'ii r.a.
kuwa Mtume s.a.w. alimuandikia 'Amri bin
Haazim r.a. wakati yuko Nijran:
"Sali mapema Sala ya Idi Adh-ha na
akhirisha Sala ya Idi Alfi'tri". Amesema Ibnu Qudaamah r.a. kuwa hivyo ni
kwa ajili ya kuupa nafasi zaidi muda wa kuchinja (kwenye Idi Adh-ha) na kuupa
nafasi zaidi muda wa kujuzu mtu kutoa Zaka (kwenye Idi Alfi'tri) inayomlazim.
Raka'a na Takbira Zake
Sala ya Idi husaliwa raka'a mbili, kwenye raka'a ya mwanzo
baada ya takbiiratu-l-ihraam (takbiira ya kuingia kwenye Sala), yaani الله أكبر
hukabbiri mara saba kabla ya kusoma Alhamdu. Kwenye
raka'a ya pili, hukabbir mara tano kabla ya kusoma Alhamdu. Hivi kama alivyo
hadithia Imam Al Tirmidhy r.a:
"Mtume s.a.w. alikabbir kwenye Sala ya Idi - katika
raka'a ya mwanzo, alikabbir takbiira saba kabla ya kusoma Alhamdu na katika
raka'a ya pili, alikabbir takbiira tano kabla ya kusoma Alhamdu".
Inasuniwa baina ya takbiir na takbiir asite muda mchache,
kiyasi cha kusoma Aya ya Qur'ani ya kiyasi; ili katika muda huo aseme:
Imepokewa hivi - kwa qauli na kitendo - kutoka
kwa Ibni Masoud r.a.
Sura za Kusomwa Kwenye Sala ya Idi
Mtume s.a.w. kwenye raka'a ya mwanzo husoma Surat "Ù‚" raka'a ya pili s.a.w. husoma Surat . Au husoma kwenye raka'a ya
mwanzo Surat na kwenye raka'a ya pili husoma Surat .
Khutba Baada ya Sala
Tafauti na Sala ya Ijumaa, khutba ya Sala ya Idi huwa baada
ya Sala; kwanza husaliwa kisha ndio Imam hukhutubu. Sunna baada ya Sala khutba
mbili (kama vile ilivyo kwenye Sala ya Ijumaa), hivi ndivyo alivyo hadithia
Imam Al Bukhary na Muslim r.a. kutoka kwa Ibni 'Umar r.a. kwamba Mtume s.aw.,
na Sayyidna Abu Bakar r.a. na Sayyidna 'Umar r.a. walikuwa wakisali Sala ya Idi
kabla ya khutba. Inapendekezwa kuianza khutba kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu
Mtukufu, kwani Mtume s.a.w. alikuwa akianza khutba zake zote kwa kumshukuru
Mwenyezi Mungu Mtukufu, haikuthibiti kuwa s.a.w. akianzia khutba za Idi kwa
takbiir, bali alikuwa akikabbir ndani ya khutba, baina ya wakati na wakati.
(Imehadithiwa na Ibnu Maajah).
Sala ya Idi Kusaliwa Jangwani/Uwandani
Ni sunna Sala ya Idi isaliwe jangwani, kwani hivi ndivyo
alivyodumisha Mtume s.a.w. kufanya. Mtume s.a.w. alisali Sala ya Idi msikitini
kwa sababu ya mvua. Imepokewa kutoka kwa Abi Huraira r.a. kwamba:
"Ilikunya mvua siku ya Idi, Mtume s.a.w. akasali nao
Sala ya Idi msikitini". (Imehadithiwa na Abu Daud na Ibnu Maajah na Al
Haakim).
Ikiwa Sala inasaliwa Makka, basi kusaliwa ndani ya Msikiti
wa Makka hapana shaka ni bora zaidi.
Kukabbir Siku ya Idi
Inapendekezwa kukabbir tangu kutua jua usiku wa kuamkia Idi
Alfi'tri mpaka kukiqimiwa Sala ya Idi. Kukabbir huku ni kwa kila mtu, mwanamke,
mwanamme, mtumzima, mtoto; akiwa njiani, akiwa sokoni, usiku na mchana, akiwa
safarini au akiwa nyumbani. Hivi ni kwa Qauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, yenye
maana ya kukusanya, yaani haikhusisha:
"….ili mumtukuze Mwenyezi
Mungu kwa alivyo kuongoeni…….". (Al Hajj : 37).
Na amehadithia Imam Al Bukhary r.a. kutoka kwa Ummu
'A'tiyah r.a.:
"Ilikuwa siku ya Idi tunaamrishwa twende kwenye Sala
ya Idi - hata waliomo kwenye hedhi - huwa nyuma ya wanaume, tukikabbir (sisi
wanawake) kwa kufuata takbiir za wanaume". Ama kukabbir siku ya Idi
Adh-ha, ni kwa Qauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:
. " ……Namna hivi tumewadhalilisha kwenu ili mumtukuze
Mwenyezi Mungu kwa alivyo kuongoeni……." (Al Hajj : 37).
Na kwa Qauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:
"Na mtajeni Mwenyezi
Mungu katika zile siku zinazo hisabiwa.......". (Al
Baqara : 203).
Imepokewa kutoka kwa Sayyidna 'Ali r.a. na Ibni ‘Abbaas
r.a. kwamba "siku zinazo hisabiwa" , , ni:
. "(Siku zinazohisabiwa)
ni tangu asubuhi ya siku ya 'Arafa, mpaka laasiri ya siku ya mwisho ya (kuwepo)
Mina".
Ibnu 'Umar r.a. alikuwa akikabbir siku zote hizi wakati
yuko Mina. Na Sayyidah Maymuna r.a. alikuwa akikabbir siku ya kuchinja " يوم النØر ". Na
wanawake walikuwa wakifuatia (wakiitikia pamoja) takbir ya Abana Ibin 'Uthman
na 'Umar bin Abdul Aziz msikitini katika siku za tashriiq. Hadithi hizi
zimekusanya kuwepo kukabbir Waislam ulimwenguni kote katika siku hizi baada ya
kila Sala ya fardhi.
Namna ya kukabbir, kama ilivyopokewa kutoka kwa Sayyidna
'Umar r.a. na Ibin Masoud r.a. ni hivi:
.
Wanaume wanatakiwa wakabbir kwa sauti kubwa, wanawake
hawatakiwi kufanya hivyo. Amesema Imam Al Bukhary r.a. kwamba Sayyidna 'Umar
r.a. alikuwa akikabbir kutoka kwenye kuba lake Mina, (kuba ni jengo lilioko juu
ya jengo, kama vile kuba la msikiti) kwa sauti wakiisikia walioko msikitini na
wao hukabbir, na hukabbir pia watu walioko sokoni; mpaka Mina yote ikitikisika
kwa sauti za takbiir.
Sala ya Kupatwa Jua na Kupatwa Mwezi
Sala ya kupatwa jua na Sala ya kupatwa mwezi ni sunna
zilizotiliwa nguvu, hivi ni kwa qauli yake Mtume s.a.w.:
"Hakika jua na mwezi havipatwi kwa mauti ya mtu au kwa
uhai wa mtu, basi mukiona hivyo; (kupatwa jua au mwezi) salini na mumuombe
Mwenyezi Mungu Mtukufu". (Imehadithiwa na Al Sheikhan).
Na kwenye riwaya nyengine: yaani muombeni Mwenyezi
Mungu Mtukufu na musali mpaka likuondokeeni lililokupateni.
Inavyosaliwa Sala ya Kupatwa Jua/Mwezi
Sala ya kupatwa jua/mwezi husaliwa raka'a mbili. Kila
raka'a kwa visimamo viwili na ruku'i mbili, kwenye kila kisimamo kwa uchache husomwa
Alhamdu. Inavyosaliwa ni hivi, huhirimia Sala
kisha atasoma Alhamdu, kisha ataruku'i, kisha
atainuka kutoka kwenye ruku'i na atasoma tena Alhamdu, kisha ataruku'i mara ya
pili, kisha itainuka kutoka kwenye ruku'i, atatua kidogo nae kasimama, kisha
atasujudi. Hii itakuwa ni raka'a moja; atasali raka'a ya pili namna alivyoisali
hii raka'a ya mwanzo. Ama ukamilifu wa Sala hii, baada ya du'a ya kufungulia
Sala - kwenye qiyamu (kisimamo) cha kwanza, akisha soma Alhamdu asome Surat Al
Baqara; kwenye qiyamu cha pili (katika hii hii raka'a ya mwanzo), akisha soma
Alhamdu asome kiyasi ya Aya mia mbili za hii Surat Al Baqara. Kwenye qiayamu
cha tatu, yaani qiyamu cha kwanza cha raka'a ya pili, akisha soma Alhamdu asome
kiyasi ya Aya mia na khamsini za Surat Al Baqara, kwenye qiyamu cha nne (raka'a
ya pili), akisha soma Alhamdu asome kiyasi ya Aya mia za hii hii Surat Al
Baqara. (Imehadithiwa na Al Sheikhan).
Imependekezwa kurefusha ruku'i ya mwanzo kwa kusabbih
kiyasi ya kusoma Aya mia za Surat Al Baqara, na kwenye ruku'i ya pili kurefusha
ruku'i kwa kusabbih kiyasi ya kusoma Aya thamanini za Surat Al Baqara; na
kwenye ruku'i ya tatu kiyasi ya kusoma Aya sabiini za Surat Al Baqara, na
kwenye ruku'i ya nne vilevile atarefusha kwa kusabbih kiyasi ya kusoma Aya khamsini
za Surat Al Baqara. Na kwenye kusujudi hurefusha kwa kiyasi kile anachorefusha
katika kila ruku'i. Hivi ni kama ilivyoelezwa na Al Sheikhan r.a. kutoka kwa
Ibni 'Abbaas r.a.:
"Lilipatwa jua siku za Mtume s.a.w., akasali s.a.w.
pamoja na watu, akasimama s.a.w. qiyam kirefu kiyasi ya kusoma Surat Al Baqara,
kisha akaruku'i ruku'i ndefu, kisha akainuka kutoka kwenye ruku'i, akasimama
qiyam kirefu, lakini kifupi kuliko cha mwanzo, kisha akaruku'i ruku'i ndefu,
lakini fupi kuliko ya mwanzo; kisha akasujudi. Kisha akasimama qiyam kirefu,
lakini kifupi kuliko cha mwanzo; kisha akaruku'i ruku'i ndefu, lakini fupi
kuliko ya mwanzo, kisha akainuka kutoka kwenye ruku'i akasimama qiyam kirefu,
lakini kifupi kuliko cha mwanzo, kisha akaruku'i ruku'i ndefu, lakini fupi
kuliko ya mwanzo, kisha akasujudi; kisha akaondoka na jua lishaachiwa".
Jama'a ya Sala ya Kupatwa Jua/Mwezi
Sala ya kupatwa jua/mwezi husaliwa jamaa, ikiwa mtu kakawia
akamuwahi Imam kwenye ruku'i ya mwanzo ya raka'a ya kwanza au raka'a ya pili
basi huwa imeiwahi raka'a hio (ya mwanzo au ya pili), lakini akimuwahi Imam
kwenye ruku'i ya pili ya raka'a ya mwanzo au raka'a ya pili huwa hakuiwahi hio
raka'a, ya kwanza au ya pili. Inapendekezwa kusaliwa kwa sauti Sala ya kupatwa
mwezi na bila ya sauti kwa Sala ya kupatwa jua.
Khutba za Sala ya Kupatwa Jua / Mwezi
Imesuniwa khutba mbili baada ya Sala ya kupatwa jua/mwezi
kama vile khutba ya Sala ya Ijumaa, lakini khutba huwa baada ya Sala kama vile khutba
za Sala ya Idi mbili; hivi ndivyo alivyokuwa akifanya Mtume s.a.w. (Imehadithiwa na Muslim).
Katika haya alisimama Mtume s.a.w. akakhutubu
"Alisimama (Mtume s.a.w.) akakhutubia, akamsifu
Mwenyezi Mungu Mtukufu, mpaka akafika akasema: "Enyi Umma wa Muhammad!
Yuko miongoni mwenu mwenye wivu zaidi ya Mwenyezi Mungu Mtukufu kumuona mja
wake, mwanamme au mwanamke wanazini"? "Enyi Umma wa Muhammad! Wallahi
lau mngaliyajuwa ninayoyajuwa mimi mungalilia mno na mungalicheka kidogo mno.
Jueni, nimefikisha ujumbe".
Imesuniwa kwenye khutba kuhimiza kuwacha huru na kutoa
sadaqa na kuhadharisha kupuuza maamrisho ya Mwenyezi Mungu Mtukufu na kuingia
kwenye ghururi. Imehadithiwa kwenye Sahih Al Bukhary kwamba Mtume s.a.w. katika
khutuba ya kupatwa jua aliamrisha kuwacha huru.
Imesuniwa wakati wa ma'saaib na mitihani ya Mwenyezi Mungu
Mtukufu kuzidi kuomba du'a na kwa unyenyekevu mkubwa, kama vile wakati wa
kupatwa na zilzala, kimbunga, upepo mkali, ukosefu wa mvua, au kuteremkiwa na
mvua kubwa na kuleta mafuriko, yote haya inahitaji kuomba du'a, kuomba maghfira
na kurejea kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa unyenyekevu mkubwa. Amesema Mwenyezi
Mungu Mtukufu:
. "Kwa nini
wasinyenyekee ilipo wafika adhabu yetu?....". (Al An'aam : 43).
Katika kuomba du'a na maghfira wakati wa ma'saaib,
inapendekezwa mtu asali nyumbani kwake, ili asiwe miongoni mwa wenye
kughafilika. Mtume s.a.w. ilikuwa ukivuma upepo mkali husema:
"Mwenyezi Mungu Mtukufu hakika mimi ninakuomba kheri
yake na kheri iliyomo ndani yake na kheri uliopelekewa; na najilinda Kwako na
shari yake na shari iliyomo ndani yake na shari uliopelekewa. Mwenyezi Mungu
Mtukufu ujaalie uwe upepo taratibu wala usiwe upepo wa nguvu".
Sala ya Kuomba Mvuwa
Sala hii husaliwa wakati inapoadimika mvuwa na kuingia
ukame, husaliwa kumuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu atujaalie mvuwa na atuondolee
ukame. Sala hii ni sunna yenye kutiliwa nguvu.
Amehadithia Imam Muslim r.a.:
"Mtume s.a.w. alikwenda kusali Sala ya kuomba mvuwa,
akawapa watu mgongo na akaelekea qibla na akakigeuza (ridaa) kitambaa chake
anachoweka mabegani". Na ameongeza Imam Al Bukhary r.a. katika riwaya
yake, yaani katika raka'a mbili za Sala hii akasoma
kwa sauti.
Kuomba Mvuwa kunakuwa kwa Njia Tatu
Uchache wake ni kwa kuomba du'a, ama mtu peke yake au watu
kukusanyika na wakaomba kwa pamoja. Ya kati yake ni kuomba du'a baada ya Sala,
hata ikiwa kwa Sala ya sunna; na katika hali hii vile vile hufuatiwa na khutba.
Na ya ukamilifu wake ni kuomba kwa kusali, kisha kufuatiwa na khutba. Kwenye
khutba Imam huwaadhi watu na kuwaonya juu ya adhabu ya Mwenyezi Mungu Mtukufu
na kuwakumbusha matokeo ya kumuasi Mwenyezi Mungu Mtukufu na kuwaamrisha kutoa
sadaqa na kila njia ya kutenda wema na kuepukana na dhulma na kuwahimiza
kutubia kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kuomba maghfira, kwani maovu ndio sababu
ya kukatika mvua na kukauka mito na kuenea ukame nchini na ni sababu ya
kuondolewa sababu ya riziki. Vilevile huwazindua kuwa kwa maasi ndio
huteremshwa adhabu ya Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa waja wake na kuenea baina yao
khofu, njaa na upungufu wa kipato na mali na mimea na mazao, hufika hata
kuangamizwa kitongoji kizima. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
"Na pindi tukitaka
kuuteketeza mji huwaamrisha wale wenye starehe na taanusi, lakini wao huendelea
kutenda maovu humo. Basi hapo kauli huthibiti juu ya mji huo, nasi
tukauangamiza kwa maangamizo makubwa".(Al Israai : 16).
Na awaamrishe kufunga siku tatu mfululizo, kisha siku ya
nne watoke nao wamo kwenye saumu; kwani du'a ya mwenye kufunga iko karibu mno
na kutakabaliwa. Watoke nao wamevaa nguo mbovu-mbovu, wawe katika hali ya wenye
kuomba, na watoke kwa upole na unyenyekevu kimya kimya bila sauti, wawe
wanyenyekevu katika mwendo wao, katika kuzungumza kwao na katika kukaa kitako kwao.
Amehadithia Abu Daud r.a. kwamba Mtume s.a.w.:
"Mtume s.a.w. alitoka (kwenda kwenye Sala ya kuomba
mvua) hali ya kuwa ni mwenye kuvaa nguo dhalili na mwenye kunyenyekea (akenda)
mpaka mahala pa kusalia". Wala hawajitii manukato, kwani manukato ni alama
ya furaha. Na inatakikana iwe Sala ya kuomba mvuwa inahudhuriwa zaidi na
watuwazima, vizee; wake kwa waume na watoto wadogo, kwani wao du'a zao ziko
karibu zaidi kutakabaliwa. Hivi ni kwa qauli ya Mtume s.a.w.:
. "Kwani munaruzukiwa
na kunusuriwa isipokuwa ni kwa ajili ya wanyonge wenu". (Imehadithiwa na
Al Bukhary). Na itahadhariwe kuwaombea mvuwa watu madhaalim na waovu, kwani hio
mvua ikija huwa ni ziada ya naqma juu yao. Sala ya kuomba mvua husaliwa kama
inavyosaliwa Sala ya Idi, husoma Imam kwa sauti na husoma Sura zile zinazosomwa
katika Sala ya Idi. Amesema Imam Shafi'ii r.a. kuwa wakati wa Sala ya kuomba
mvua ni ule wakati unao saliwa Sala ya Idi, na imesemwa kuwa haina wakati
maalum. Akimaliza kusali, atasoma khutba mbili, kwani Mtume s.a.w. alisoma khutba ya Sala ya kuomba mvua
nae s.a.w. yuko juu ya membari.
Amesema Abu Huraira r.a
"Mtume s.a.w. alitoka kuomba mvuwa, akasali pamoja na
sisi raka'a mbili bila ya adhana wala iqama, kisha akatukhutubia na akamuomba
Mwenyezi Mungu Mtukufu. Akaelekea qibla na akainua mikono, akaigeuza ridaa
yake, akajaalia kuliani kuwa kushotoni na kushotoni kuwa kuliani".
(Imehadithiwa na Ahmad na Ibnu Maajah na Al Bayhaqy).
Katika hii Sala ya kuomba mvua huzidishwa kuomba maghfira
kwenye khutba ya kwanza na ya pili, kwani kuomba maghfira ndilo khasa lenye
kutakikana katika hali hii, hali ya kushukiwa na ghadhabu ya Mwenyezi Mungu
Mtukufu. Na itahadhariwe mwisho wa hadhari, kuomba maghfira kwa ulimi, na hali
moyoni haimo nia khasa, bali moyo bado umo katika kuendelea na maasi na jeuri
na dhulma na kuacha kufuata maamrisho ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, na kuwafanyia
khiana raia; kwani haya yatazidisha ghadhabu za Mwenyezi Mungu Mtukufu. Hivyo
ni kwa vile mwenye kujidai kutubia nae akawa anazidi kuzama kwenye uovu na maasi
ni kumfanyia istihzai Mwenyezi Mungu Mtukufu; na katika hali hio; wapi
itatarajiwa kupata kukubaliwa du'a. Imepokewa kwamba Sayyidna 'Umar r.a. wakati
alipoomba mvuwa hakuongeza isipokuwa kuomba maghfira. Wakasema watu: "Ewe
Amir-l-Muuminiin!" Hatukukuona kuomba mvuwa? Akasema Sayyidna 'Umar r.a.:
"Nimeomba mvua kwa michirizi ya mbinguni yenye kunyeshesha mvua".
Kisha akasoma:
. "…: Ombeni msamaha kwa Mola wenu Mlezi; hakika Yeye ni
Mwingi wa kusamehe. Atakuleteeni mvua inyeshe mfululizo". (Nuh : 10-11).
Waarabu katika jaahilia walikuwa wakiamini kuwa kuna nyota
ndizo zenye kunyeshesha mvuwa, Sayyidna 'Umar r.a. akawaambia kuwa kinacho
nyeshesha mvuwa ni kuomba maghfira kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, si nyota; na
hicho ndicho alichoombea yeye. Kisha Sayyidna 'Umar r.a. huigeuza ridaa yake,
na watu nao hufanya kama anavyofanya yeye Sayyidna 'Umar r.a., hivi ndivyo
ilivyohadithiwa na Abu Huraira r.a.
Hivi kugeuza ridaa ni kuashiria kugeuka hali, kutoka katika
taabu kuingia kwenye raha; na kutoka kwenye shida kuingia kwenye wepesi na
kutoka kwenye ghadhabu za Mwenyezi Mungu Mtukufu kuingia kwenye maghfira na
ridhaa Zake Mwenyezi Mungu Mtukufu. Kisha huinua mikono na kuomba kwa du'a
aliokuwa akiomba Mtume s.a.w., na huenda
mno kwenye kuomba kisirisiri na kwa sauti, hivi ni kufuatana na Qauli ya
Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Muombeni Mola wenu Mlezi kwa unyenyekevu na kwa
siri.....". (Al
'Araaf : 55).
Ikawa anapoomba kwa siri na watu nao huomba (kwa siri),
anapoomba kwa sauti watu huitikia, Amin.
Ifuatayo ndio du'a aliokuwa akiomba Mtume s.a.w. katika
Sala ya kuomba mvuwa:
Maana ya Hadithi/dua hii ni kama hivi: "Mwenyezi Mungu
Mtukufu, tunyeshee mvuwa ya rehma si mvuwa ya adhabu, wala ghadhabu, wala
balaa, wala isiwe mvuwa yenye kubomowa, Mwenyezi Mungu Mtukufu mwenye kuinua
majabali na milima, na maoteo ya miti na matumbo ya mito, Mwenyezi Mungu
Mtukufu, tujaalie iwe mvuwa yenye kutuzunguka kwa neema si yenye kutumiminikia
na madhara. Mwenyezi Mungu Mtukufu tujaalie iwe mvuwa yenye kuondowa shida,
yenye wingi wa maji, yaenee kwenye ardhi na miti, ituwe na izame kwenye ardhi
na idumu nafuu yake. Mwenyezi Mungu Mtukufu tuteremshie mvuwa, wala usitujaalie
wenye kukata tamaa na Rehma Zako. Mwenyezi Mungu Mtukufu wanusuru waja wako na unusuru
mji kutokana na ukame na shida zake, na utunusuru na njaa, na utunusuru na
dhiki ambayo hatuna kwa kushitaki isipokuwa Kwako Mola wetu Mlezi, kwani ni
Wewe Pekee ndie mwenye uwezo wa kutuletea neema na kutukinga na kila balaa.
Mwenyezi Mungu Mtukufu, tuoteshee konde zetu, na utuzidishie unyenyekevu, na
ututeremshie barka za mbinguni, na utuoteshee kutokana na barka za ardhi, na
utuondolee balaa ambazo hapana wa kutuondolea isipokuwa ni Wewe Mola wetu
Mlezi. Mwenyezi Mungu Mtukufu tunakuomba maghfira, kwani Mola wetu Mlezi daima
ni mwenye kutughufiria, tunakuomba utughufirie na ututeremshie mvuwa inyeshe
mfululizo". (Imehadithiwa na Imam Shafi'ii r.a. kutoka kwa Salim bin
Abdullah r.a.).
Inapoteremka mvuwa na maji kupita kwenye mabonde inasuniwa
kujitilia udhu na/au kukoga. Imesemwa kwenye Al Majmu'i kwamba watu wakisikia
ngurumo za radi waseme:
. "Ametakasika Mwenyezi
Mungu Mtukufu ambae radi humsabbih kwa kumhimidi na Malaika kwa
kumukhofu". (Imehadithiwa na Imam Malik).
Na kukimwesa (ukipiga umwesa) imesuniwa kusema:
. "Ametakasika
Mwenyezi Mungu Mtukufu anaekuonesheni umwesa, na mkawa katika khofu na
tamaa". Inapendekezwa kukimwesa usifuatishie macho yako umweso, kwani
wanazuoni waliotangulia walikuwa wakichukia kufanya hivyo na walikuwa wakisema
kunapomwesa:
. Maana yake ni kama hivi:
"Hapana anaepasa kuabudiwa kwa haqi isipokuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, hana
mshirika. Mwingi wa kutakasika na Mwingi wa kutukuzwa". Amesema Al Marwady
inapendeza kufuata hivi walivyokuwa wakifanya hao wanazuoni waliotangulia. Na
imependekezwa kusema wakati inaponyesha mvua: , yaani Mwenyezi Mungu
Mtukufu tujaalie mvua kubwa na yenye manufaa. (Imehadithiwa na Al Bukhary).
Akishasema hivi aombe lile analolitaka. Hivi ni kwa vile
alivyoeleza Al Bayhaqy r.a. kwamba du'a huitikiwa zaidi katika hali nne, wakati
wa mapigano (vita) baina ya washirikina na Waumini, na wakati inaponyesha mvua,
na wakati inapoqimiwa Sala, na unapoiona Al Ka'aba.
Na imependekezwa kusema inaposita mvuwa:
. "Tumeteremshiwa
mvuwa kwa fadhila za Mwenyezi Mungu Mtukufu juu yetu na Rehma Zake kwetu".
Ni karaha kutukana (kuulani) upepo, bali ni sunna kuomba
du'a wakati ukivuma upepo kwa Hadithi ya Mtume s.a.w.:
"Upepo ni miongoni mwa Rehma za Mwenyezi Mungu
Mtukufu, huja kwa rehma na huja kwa adhabu, basi mukiuona musiutukane
(musiulaani), na muombeni Mwenyezi Mungu Mtukufu kheri za huo upepo, na
mujilinde na Mwenyezi Mungu Mtukufu na shari za huo upepo". (Imehadithiwa
na Al Bayhaqy).
Amesema Imam Shafi'ii r.a. kumwambia Aba Bakry Al Waraq
r.a.: "Nielimishe kitu kitakacho nikaribisha kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu na
kitakacho ni weka mbali na watu". Akasema kunambia: "Ama kitakacho
kuweka karibu kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu ni kumuomba, na kitakacho kuweka mbali
na watu ni kuwaomba". Kisha imepokewa na Abu Huraira r.a. kwamba Mtume
s.a.w. kasema: . "Asiye muomba
Mwenyezi Mungu Mtukufu, basi Mwenyezi Mungu Mtukufu humghadhibikia". Kisha
akasoma beiti hizi:
Maana ya beiti hizi ni kama hivi: "Kabisa usimuombe
binaadam kitu Na muombe Ambae milango Yake haifungwi Mwenyezi Mungu
hughadhibika ukiwacha kumuomba Na binaadam unapo muomba hughadhibika".
Sala katika Wakati wa Khofu
Sala ya khofu imekuja katika Sharia kwa Qauli ya Mwenyezi
Mungu Mtukufu, Hadithi za Mtume s.a.w. na itifaqi ya wanazuoni.
Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
"Na unapo kuwa pamoja nao,
ukawasalisha, basi kundi moja miongoni mwao wasimame pamoja nawe na wachukue
silaha zao ....". ( Annisaai : 102 ).
Na qauli ya Mtume s.a.w.: . "Salini kama
mnavyoniona mimi nnasali". Na Mtume s.a.w. ameisali Sala ya khofu na
wameisali Masahaba r.a. baada yake, ikawa ni itifaqi ya wanazuoni; na kwa vile
sababu yake bado ingalipo, hufanywa kama Sala ya kufupisha, na inajuzu kusaliwa
na mkaazi (muqim) au msafari.
Hali na namna inavyosaliwa Sala ya Khofu
Sala ya khofu husaliwa katika hali na namna tatu:
Ya Kwanza, yakuwa adui hayuko upande wa qibla. Imam atawagawa maamuma
makundi mawili, kundi litasimama kujikinga na adui, na kundi la pili litaqim
Sala na kusali pamoja na Imam raka'a moja kaamil, yaani mpaka kumaliza sijda.
Atapoinuka Imam kutoka kwenye sijda kwenda raka'a ya pili, maamuma wataacha
kumfuata kwa nia ya kumuacha Imam na watamaliza Sala yao - raka'a ya pili -
wenyewe, yaani bila ya Imam na watakaa tahiyatu na kutoa salam, na watakwenda
upande alioko adui, kumkinga adui na wenziwao. Hapa tena litakuja lile kundi
ambalo lilikuwa likielekeana na adui na kuja kusali na Imam, wakati Imam yuko
kwenye raka'a ya pili; na Imam atarefusha qiyam mpaka ili waweze hawa maamuma
kumuunga yeye Imam katika hio raka'a ya pili, wakishamuunga Imam hao maamuma
wote hapo tena Imam atasali hio raka'a ya pili. Imam akikaa kwenye tahiyatu
katika hii raka'a ya pili, wao maamuma watainuka na kutimiza raka'a yao ya
pili, wakati huu Imam hatatoa salam, bali atangoja mpaka na hawa maamuma wakae
tahiyatu na wawahi kusoma du'a ya tahiyatu, ikisha Imam atatoa salam pamoja
nao. Sala hii ndivyo khasa alivyosali Mtume s.a.w. walipokua Dhaat Riqa'i (yenye viraka).
Dhaati Riqa'i, ni mahala katika Najdi; pamepewa jina hili kwa sababu Mtume s.a.w. na Masahaba zake r.a. walifunga miguu
yao (nyayo) kwa vitambaa kwa kupasuka miguu yao kutokana mwendo mrefu.
Ya Pili, yakuwa adui yuko upande wa qibla. Imam atawapanga maamuma
safu mbili, wote kwa pamoja watahirimia Sala na watasali pamoja mpaka wainuke
kutoka ruku'i ya raka'a ya kwanza, hapo tena safu moja itakwenda kwenye
kusujudi pamoja na Imam, watasujudi pamoja na Imam, kisha watainuka pamoja na
Imam mpaka kwenye qiyam cha raka'a ya pili, hapo ile safu ya pili itakwenda
kwenye kusujudi, itasujudi kisha watainuka na kukutana na Imam na ile safu ya
kwanza kwenye raka'a ya pili, watasoma pamoja, na wataruku'i pamoja, wakiinuka
kutoka kwenye ruku'i wakifika kwenye qiyam, wale waliosujudi mwanzo watalinda
na wale wa safu ya pili watakwenda kwenye kusujudi, wakiinua vichwa kutoka
kwenye kusujudi wale walimo kwenye kulinda watakwenda kwenye kusujudi. Sala hii
ndivyo alivyosali Mtume s.a.w. walipokua
'Asfaan, kama ilivyo hadithiwa na Abu Daud na wengineo. Sala ya namna hii ina
shuruti tatu:
Kwanza,
awe adui upande wa qibla.
Pili,
awe adui juu ya jabali au pahala palioinuka, hafichiki, yaani Waislam wanawaona
vyema hao maadui.
Tatu, iwe
idadi ya Waislam ni yenye kutosha kuwa na kundi la kusali na kundi la kulinda.
Namna ya Tatu, wakati vinapo pambamoto vita na kuzidi khofu, katika hali
hii haiwezekani kugaiwa Mujaahidiina makundi mawili, hapo kila mtu husali peke
yake, ikiwa anakwenda kwa miguu au ikiwa yuko juu ya kipando, ikiwa ameelekea
qibla au hakuelekea qibla. Hivi ni kwa Qauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Ikiwa mnakhofu (Salini) na
hali mnakwenda kwa miguu au mmepanda……". (Al Baqara : 239).
Amesema Ibnu 'Umar r.a. yaani ikiwa mwenye kuelekea qibla au
hakuelekea qibla. (Imehadithiwa na Malik).
Amesema Imam Shafi'ii r.a. kuwa katika hali hii Sala
husaliwa kama inavyo wezekana, muhim hapana kuakhirishwa Sala, wala Sala hii
hailipwi. Huwemo ndani yake mambo mengi yenye kuambatana na vita, kama vile
dharba za panga na mikuki za mfululizo, lakini juu ya hivyo hairuhusiwi wakati
wa kusali kupiga siyahi kwa vile hakuna sababu ya kufanya hivyo. Ikiwa katika
Sala hii haiwezekani kuruku'i au kusujudi, basi huashiria hio ruku'i na sijida,
atajaalia sijida kuinama zaidi kuliko ruku'i; isipowezekana kufanya hata hivi,
basi atasali kwa namna yoyote ile inayowezekana. Muhim Sala isiakhirishwe
kufika nje ya wakati wake.
0 comments:
Post a Comment