Monday, December 8, 2014

DALILI ZA KUKARIBIA KWA SIKU YA QIYAAMAH

Mwenyezi Mungu Amemleta Mtume wake Muhammad (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akiwa kama ni mletaji habari njema na muonyaji ambaye hakuacha jambo lolote la kheri isipokuwa ametujuulisha nalo na kutuhimiza kulikimbilia, na hakuacha jambo lolote la shari isipokuwa ametutahadharisha nalo.


Na kwa vile Ummah huu ni Ummah wa mwisho, basi Mtume huyu mtukufu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) ametuletea kutoka kwa Mola wake dalili za kutosha zilizo wazi, zenye kutujuulisha juu ya kukaribia kwa Siku ya Qiyaamah. Akatubainishia kwa ulimi wake, tena kwa ufasaha kabisa, juu ya baadhi ya yatakayotokea katika mwisho wa zama. Akatuhakikishia kuwa yote hayo lazima yatatokea, haya yote yakiwa ni dalili juu ya ukweli wa Utume wake (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) utakayowafanya watu wajitayarishe vizuri na Siku hiyo. Siku ambayo mtu hatovuna isipokuwa kile alichochuma, na hatokuwa na wakumlaumu isipokuwa nafsi yake.

Mwenyezi Mungu Anasema:

{{“Isije ikasema nafsi (asije akasema mtu); “Eee majuto yangu kwa yale niliyopunguza upande wa Mwenyezi Mungu, na hakika nilikuwa miongoni mwa wanaoyafanyia mzaha (mambo ya diyn)”.



Au ikasema; “Kama Mwenyezi Mungu angeniongoa bila shaka ningekuwa miongoni mwa wenye kumcha Mwenyezi Mungu”.

Au ikasema ionapo adhabu; “Kama ningepata marejeo  (ya kurejea tena duniani) ningekuwa miongoni mwa wafanyao mema”.

(Ataambiwa) “Kwa yakini! Bila shaka zilikujia Aayah (dalili) zangu ukazikadhibisha na ukajivuna na ukawa miongoni mwa wanaotakabari”.}}

[Az-Zumar: 56-59]

Katika kuzijua dalili hizo kisha kuziona zikitendeka hapa duniani kunampatia mtu faida nyinigi sana zikiwemo zifuatazo:

·         Kuwa na uhakika juu ya ukweli wa Utume wake Muhammad (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam).
·         Kujitayarisha vizuri na Siku ya Qiyaamah. Kwani kwa mfano mtu   anapopewa habari juu ya meli inayokaribia kuwasili bandarini, huingoja        meli hiyo huku akiwa na wasi wasi mwingi. Lakini anapoisika sauti ya         selo ya meli hiyo, anakuwa na uhakika usio na shaka kuwa meli sasa   imekaribia kweli kuwasili.

Mfano huu ni sawa na mtu aliyejuulishwa juu ya dalili ya kukaribia kwa Siku ya Qiyaamah, kisha akaziona dalili hizo zikitendeka mbele ya macho yake kama zilivyoelezwa na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam). Mtu huyo anakuwa na uhakika usio na shaka wa kuwepo kwa siku ya Qiyaamah.

·         Kwa ajili hiyo, kuzijua na kuziona dalili za kukaribia kwa Siku ya    Qiyaamah kunaongeza pia yakini juu ya ukweli wa kukaribia kwa Siku hiyo.
·         Kunamsaidia mtu kutoyumbishwa na masaibu, mitihani na machafuko    yanayotekea kila siku. Kwani akirudi katika mafundisho ya Mtume wa      Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) ataona kuwa yote hayo yamekwishatajwa kuwa yatakuja kutokea.
·         Kunamsaidia mtu aliyejisahau akawa anaikimbilia dunia, anapoziona       dalili hizo zikitokea kikweli humkumbusha mtu huyo akawa anaifanyia          kazi Akhera yake badala ya kuikimbilia dunia.

Kutokana na haya na mengi mengineyo, Mwenyezi Mungu Akamfunulia Mtume wake (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) baadhi ya dalili ya yale yatakayotokea kabla ya kuja kwa Siku ya Qiyaamah.

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alikuwa anapozungumza juu ya dalili za kukaribia kwa Siku ya Qiyaamah, mashavu yake yanageuka kuwa mekundu huku akiipaza sauti yake juu kwa ghadhabu mfano wa Amiri Jeshi mwenye kulipa amri jeshi lake.

<iframe width="420" height="315" src="//www.youtube.com/embed/x8IOJ89vAGA" frameborder="0" allowfullscreen></iframe>


Alikuwa pia akisema:

((“Nimeletwa baina yangu na Qiyaamah kiasi kama hiki”, huku akiashiria kwa kidole chake cha shahada na cha pili yake.))

Zipo dalili zinazoitwa ‘dalili ndogo’ na zipo pia ‘dalili kubwa’ za Siku ya Qiyaamah. Nyingi katika dalili ndogo zimekwisha tokea na kuonekana, jambo lililowafanya Waislamu waongezeke imani na kumsadiki zaidi Mtume wao (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam). Wakati zitakapoanza kuonekana dalili kubwa, basi zitatunga na kufuatana moja baada ya nyingine mpaka Qiyaamah kitakaposimama. Lakini sisi tutazitaja hapa baadhi yake na chache sana miongoni mwa ‘dalili ndogo’ tu.


Fitan

Neno ‘Fitan’ ambalo ni wingi wa (plural ya) Fitnah; maana yake ni Mitihani. Lakini neno hili linaongezeka maana yake kila linapozidi kutumika. Kwani neno hili linaweza kumaanisha misiba, madhambi, kufru, mauaji, kuchomwa moto n.k.

Neno ‘Fitan’ pia linamaanisha vita vya wenyewe kwa wenyewe (civil wars). Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) ametujuulisha juu ya Fitnah nyingi sana zitakazotokea baada yake zikiwa kama ni dalili ya kukaribia kwa Siku ya Qiyaamah. Fitnah zitakazomfanya mtu asiweze kutambua ipi haki na ipi baatwil. Fitnah zitakazozitetemesha nyoyo na kuiyumbisha imani, hadi kufikia kwamba mtu anaweza akaamka asubuhi akiwa ni Muislamu na jioni yake akageuka kuwa kafiri, au anaweza kuamka asubuhi akiwa kafiri na jioni yake akawa Muislamu.
Kila inapotokea fitnah, mtu hudhani kuwa hii ndiyo itakayoangamiza, kisha humalizika na kutokea nyingine kubwa kuliko ile. Na hali itaendelea hivyo mpaka kitakaposimama Qiyaamah.

Anasema Abu Muusa Al-Ash’ary (Radhiya Allaahu ‘Anhu) kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:
((Kinapokaribia Qiyaamah zitatokea Fitnah nyingi mfano wa vipande vya usiku wenye kiza kizito, mtu ataamka ndani yake akiwa Muislamu na jioni yake anakuwa kafiri, au anakuwa wakati wa jioni Muislamu na asubuhi anakuwa kafiri. Aliyekaa katika mtihani huo anakuwa bora kuliko aliyesimama, na aliyesimama anakuwa bora kuliko mwenye kutembea taratibu, na mwenye kutembea anakuwa bora kuliko anayekwenda mwendo wa kukazana.)) [Imepokewa na Imaam Ahmad, Ibni Maajah, Al-Haakim na wengineo]

Imetolewa na Muslim pia kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘Anhu) kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) amesema: ((Kimbilieni kufanya ‘amali njema kabla ya kuja kwa Fitnah mfano wa vipande vya usiku wenye kiza kizito, mtu ndani yake anaamka akiwa Muislamu na jioni yake anakuwa kafiri, au jioni anakuwa kafiri na asubuhi anakuwa Muislamu. Mtu ndani ya Fitnah hizo anaiuza diyn yake kwa thamani ndogo ya dunia.)) [Imepokewa na Muslim]

Na maana ya neno ‘vipande vya usiku wenye kiza kizito’, ni ule ubaya wa Fitnah hizo utakaomfanya mtu achanganyikiwe asiweze kutambua baina ya haki na baatwil.

Kutoka kwa Ummu Salamah (Radhiya Allaahu ‘Anha) amesema kuwa usiku mmoja Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) aliamka akiwa na hofu nyingi huku akisema: ((Subhaana Llaah! Hazina ngapi alizoteremsha Mwenyezi Mungu, na mitihani mingapi aliyoiteremsha Mwenyezi Mungu? Nani atakayewaamsha waliolala vyumbani mwao (akimaanisha wake zake), huenda mtu akawa amevaa duniani akaenda uchi Akhera.))

Maulamaa wamelitafsiri neno ‘amevaa duniani akaenda uchi Akhera’, tafsiri nyingi sana zikiwemo zifuatazo:

·         Mtu tajiri mwenye nguo nyingi hapa duniani lakini hana ‘amali njema za           kumsitiri huko Akhera.
·         Wengine wakasema kuwa maana yake ni mtu mwenye kuvaa nguo
zisizomsitiri hapa duniani na huko Akhera hatokuwa na cha kumsitiri.


Kuvunjwa Kwa Mlango

Nitaanza kwa kutaja baadhi ya Hadiyth alizozungumzia ndani yake Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) Fitnah za mwanzo katika Uislamu, Fitnah zilizotokea miaka michache baada ya kufariki kwake, mara baada ya kuuliwa kwa Khaliyfah wa pili wa Waislamu ‘Umar bin Khatwaab (Radhiya Allaahu ‘Anhu).

Kutoka kwa Hudhayfah (Radhiya Allaahu ‘Anhu) amesema kuwa:
‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ‘Anhu) aliuliza siku moja: “Yupi kati yenu aliyehifadhi kauli ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) juu ya Fitnah?”.

Hudhayfah akasema: “Mimi nimehifadhi kama alivyosema”.

‘Umar (Radhiya Allaahu ‘Anhu) akamwambia: “Tuhadithie, kwani wewe ni jasiri”.

Hudhaifah (Radhiya Allaahu ‘Anhu) akasema: “Fitnah ya mtu katika ahli yake (watu wa nyumba yake) na mali yake na jirani zake zinaondoka kwa kuswali na kutoa Sadaka na kwa kuamrisha mema na kukataza mabaya”.

‘Umar akasema: “La, mimi sikusudii (fitnah) hizi, bali zile zinazorusha mawimbi (makubwa) kama mawimbi ya bahari”.

Akasema: “Ewe Amiri wa Waislamu! Wewe umeepukana nazo Fitnah hizo, kwani baina yako na baina yake (Fitnah hizo) upo mlango uliofungwa”.

‘Umar akauliza: “Mlango huo utafunguliwa au utavunjwa?”

Akasema: “La, bali utavunjwa”.

‘Umar (Radhiya Allaahu ‘Anhu) akasema: “Kwa hivyo hautofungika tena...” Na katika riwaya nyingine akasema: “Kwa hivyo hautofungika mpaka Siku ya Qiyaamah?”

Wakamuuliza (waliokuwa wakimsikiliza Hudhayfah baada ya kufa kwa ‘Umar): “Aliujua?” Na katika riwaya nyingine: “’Umar alikuwa akiujua mlango huo?”.

Hudhayfah (Radhiya Allaahu ‘Anhu) akawaambia: “Naam kama (anavyojua kuwa) usiku wa leo unakuja kabla ya usiku wa kesho)”.

Masruuq bin Al Ajda-a alipomuuliza Hudhayfah (Radhiya Allaahu ‘Anhu): “Nani mlango huo”.

Akasema: “(Mlango huo ni) ‘Umar.”

Kisha Hudhayfah (Radhiya Allaahu ‘Anhu) akawaambia: “Mimi nilimuhadithia ‘Umar Hadiyth (hii) kama nilivyomsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) bila makosa.”

Ikawa kama alivyotujuulisha Msemakweli Muhammad (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam), kwani mlango huo ulivunjwa mara baada ya kuuliwa Khaliyfah wa pili wa Waislamu ‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ‘Anhu). Kuanzia hapo Fitnah zikafunguka na kuenea na kukithiri, na Fitnah ya mwanzo ilikuwa kuuliwa kwa Khaliyfah wa tatu wa Kiislamu- Mwenye Nuru mbili ‘Uthmaan bin ‘Affaan (Radhiya Allaahu ‘Anhu).

[Imepokewa na Al-Bukhaariy, Muslim na At-Tirmidhiy]

Kuuliwa Kwa ‘Uthmaan (Radhiya Allaahu ‘Anhu)

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) aliwahi kumbashiria ‘Uthmaan bin ‘Affaan (Radhiya Allaahu ‘Anhu) kuwa atakumbwa na mtihani mkubwa.

Kisa chenyewe ni kama ifuatavyo:

Anasema Abu Muusa Al-Ash’ary (Radhiya Allaahu ‘Anhu) kuwa siku moja alimuona Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akielekea katika kisima kilichozungushiwa ukuta.

Abu Musa Al-Ash’ary anasema: “Nikasema: Leo mimi nitakuwa mlinzi wa Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam).” Nikamuona Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akielekea kisimani, akakidhi haja yake kisha akakaa juu ya kisima huku akining’iniza miguu yake.  

Akaja Abu Bakr akataka ruhusa ya kuingia ndani, nikamwambia: “Hapo hapo ulipo, ngoja kwanza usiingie mpaka nikakuombee ruhusa kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam)”. Nikamwendea Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) na kumwambia: “Abu Bakr anataka ruhusa ya kuingia”, Akanambia: ((Mruhusu aingie, na mbashirie Pepo)). Nikafanya hivyo, akaingia na kukaa juu ya kisima kuliani kwa Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) na kuining’iniza miguu yake kama alivyofanya Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam).

Mlango ukagongwa tena. Nikatamani mgongaji awe ndugu yangu. Nikauliza: “Nani?”, “’Umar bin Al-Khattwaab”, Nikamwambia: “Hapo hapo ulipo, usiingie mpaka kwanza nimjulishe Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam)”. Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akanambia: ((Mruhusu aingie, na mbashirie Pepo)). Nikafanya hivyo, na ‘Umar naye akaingia na kukaa juu ya kisima kushotoni kwa Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) na kuining’iniza miguu yake kama walivyofanya wenzake.

Haujapita muda mlango ukagongwa tena: Nikatamani mgongaji awe ndugu yangu. “Nani?” “‘Uthmaan bin ‘Affaan”. Nikamwambia: “Hapo hapo ulipo, usiingie mpaka kwanza nimjulishe Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam)”. Nilipomjulisha, Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akanyamaza muda kidogo, kisha akanambia: ((Mruhusu aingie na mbashirie Pepo baada ya kupambana na mtihani mkubwa)). Nilipomwambia hivyo, ‘Uthmaan akasema: “Allaahul-Musta’an”, (na katika riwaya nyingine alisema: “Tutakuwa na subira In shaa Allaah”). Kisha akaingia, lakini ‘Uthmaan hakupata pa kukaa, akaenda upande wa pili akakaa akiwa amekabiliana nao.

Anasema Abu Muusa (Radhiya Allaahu ‘Anhu): “Nikahisi kama hivi ndivyo makaburi yao yatakavyokuwa, na nikatamani ndugu yangu naye aje”.
[Imepokewa na Al-Bukhaariy]

Ingawaje ‘Umar bin Khattwaab (Radhiya Allaahu ‘Anhu) aliuliwa kama alivyouliwa ‘Uthmaan (Radhiya Allaahu ‘Anhu), lakini ‘Umar aliyeuliwa na kafiri anayeabudu moto wakati akiswalisha Swalah ya Alfajiri hakupata misukosuko kama aliyopata ‘Uthmaan (Radhiya Allaahu ‘Anhu) kabla ya kuuliwa kwake.

Baada ya kuuliwa ‘Uthmaan (Radhiya Allaahu ‘Anhu) Fitnah zikawa nyingi, khitilafu zikaongezeka, hata Maswahaabah (Radhiya Allaahu ‘Anhu) walishiriki katika vita vya wenyewe kwa wenyewe.


Mnayaona Ninayoyaona Mimi?

Siku moja alipokuwa akisimamia ujenzi wa ngome katika mji wa Madiynah, Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) aliyekuwa akiyajuwa yote hayo kuwa yatatokea, aliwauliza Maswahaba wake: ((Mnaona ninayoyaona?))

Maswahaba (Radhiya Allaahu ‘Anhum) wakasema: “Hatuoni (kitu) ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu.”

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akasema: ((Mimi naona mapigano mengi yakitokea baina ya nyumba zenu, wingi wa nyumba kubwa kubwa (zinazowakusanya watu wengi ndani yake).))


Fitnah Zitokazo Upande Wa Mashariki

Fitnah nyingi zilizowakumba Waislamu zilitokea upande wa Mashariki ya dunia, na Fitnah ya mwanzo iliyoleta mfarakano baina ya Waislamu ilitokea upande huo wa Mashariki, jambo ambalo bila shaka lilimfurahisha sana Shaytwaan. Na haya yanakubaliana na maneno ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) aliyetujuulisha kuwa huko ndiko kwenye pembe ya Shaytwaan.

Kutoka kwa Ibn ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘Anhu) amesema kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) amesema huku akiashiria upande wa Mashariki: ((Fitnah ipo huku, Fitnah ipo huku, kutakapotokeza pembe ya Shaytwaan.)) [Imepokewa na Al-Bukhaariy na Muslim]

Habari hizi alizotujuulisha Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) zilianza kuonekana tokea mwanzo wakati yalipotokea mapigano ya wenyewe kwa wenyewe, jambo ambalo bila shaka yoyote lilimfurahisha sana Shaytwaan.

Anasema Shaykh Yuusuf bin ‘Abdillaah Al-Waabil kuwa: “Kutoka upande wa mashariki Fitnah nyingi sana zilitokea. Kwani huko ndiko yalipoanza mapigano ya wenyewe kwa wenyewe baina ya Waislamu. Kutoka huko umekuja Ukadiani, Ukoministi. Matartar pia wametokea huko katika karne ya saba ya Hijriyyah, wakaangamiza na kueneza shari kubwa sana”.
“Hadi hii leo”, anaendela kusema Shaykh Yuusuf: “Fitnah zinaendelea kutujia kutokea upande huo wa Mashariki ya dunia na hata Yajuju na Majuju watatokea upande huo huo”.


Kupotea Kwa Amaanah

Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘Anhu) kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) amesema: ((Uaminifu utakapoondoka basi isubirini Sa’ah (kingojeeni Qiyaamah).)) Akaulizwa: “Vipi unapotea (uaminifu) ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu?”
Akasema: ((Mambo yakiegemezwa kwa wasiostahiki, basi isubirini Sa’ah.)) [Imepokewa na Al-Bukhaariy, Kitaabur-Riqaaq]

Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akatubainishia pia kuwa uaminifu utatoweka katika nyoyo na kubaki athari yake tu.

Imepokewa kutoka kwa Hudhayfah (Radhiya Allaahu ‘Anhu) kuwa amesema: “Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) amenihadithia mambo mawili, na mojawapo katika hayo nimekwishaliona likitokea na ninalisubiri la pili (nilione pia). Amenihadithia kuwa uaminifu utatoweka. Amenihadithia kuwa amaanah (ilipoteremshwa), iliteremshwa ndani ya mizizi ya nyoyo za watu, kisha iilipoteremshwa Qur-aan wakaijua zaidi, kisha wakaijua (vizuri zaidi) kupitia katika Sunnah (Mafundisho ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam)).”

Kisha akatuhadithia juu ya kunyanyuliwa (kupotea) kwa amaanah akasema: ((Mtu analala usingizi huku amaanah inafutwa moyoni mwake na kubaki athari yake tu, mfano wa doa lisilokuwa na rangi. Kisha analala usingizi (mwingine) na amaanah inafutwa (‘tena’ - yaani hilo doa lililobaki). Kisha itabaki amaanah mfano wa alama (ya ngozi iliyokunjika) inayobaki mkononi baada ya mtu kunyanyua kitu”, (inayotoweka baada ya kupita muda mdogo) (au) maumivu yanayobaki mguuni baada ya kukanyaga kijinga kidogo cha moto (pakafanya lenge lenge kisha likakauka).))

Kisha Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akasema: ((Kisha watu watakuwa wanafanya biashara na hapana hata mmoja kati yao atakayekuwa muaminifu, itafika hadi kusemwa; “Katika watu wa kabila Fulani yupo mtu mmoja muaminifu. Na hata itafika hadi watu watakuwa wakimsifia mtu huku wakisema: ‘Mwanamume kweli huyu, mkarimu kweli huyu, ana akili kweli huyu’, (atapewa sifa zote hizo) wakati mtu huyo hana imani (wala uaminifu) hata yenye uzito wa hardali.))

Hudhayfah (Radhiya Allaahu ‘Anhu) akaendela kusema: “Nimekwishaiona zama ambayo ndani yake uaminifu baina ya watu ulikuwepo. Na sikuwa nikijali ninafanya biashara na nani (kwa sababu watu wote waaminifu), akiwa mtu huyo ni Muislamu basi Uislamu wake utamfanya asiipoteze amaanah yake. Na kama mtu huyo ni Mkiristo au Myahudi, basi atakuwa anafanya kama anavyotakiwa (kutonidhulumu haki yangu). Ama wakati huu wa leo, uaminifu umeondoka, na khiyaanah imedhihiri na sitofanya biashara isipokuwa na fulani au fulani (tu)”.
Yaani alikuwa akifanya biashara na baadhi ya watu wachache tu alokuwa akiwaamini.

Hudhayfah (Radhiya Allaahu ‘Anhu) aliishi muda baada ya kuuliwa kwa ‘Uthmaan bin ‘Affaan (Radhiya Allaahu ‘Anhu).
[Imepokewa na Al-Bukhaariy na Muslim]

Anasema Shaykh Yuusuf bin ‘Abdillaah Al-Waabil aliyeandika kitabu cha Ashraatwus-Sa’ah kuwa: “Miongoni mwa dalili za kupotea kwa amaanah ni kule kupewa ufalme, uongozi au uhakimu watu wasiokuwa waadilifu wala waaminifu. Kwani viongozi wanapotengenea, raia nao hutengenea. Ama huko juu kukiharibika, basi chini nako kutaharibika pia. Na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) amekwishatujuulisha kuwa utafika wakati wa hadaa, mambo yatakapokwenda kinyume. Wakati huo, muongo ndiye atakayesadikiwa na mkweli atakadhibishwa, na muaminifu ataitwa haini na haini ndiye atakayeaminiwa”.

Kubebeshwa mzigo wa uongozi watu wasioijali Dini yao, ni dalili ya watu kutojali maamrisho ya Dini yao. Na dalili ya upungufu wa Ma’ulamaa na kuongezeka kwa ujinga, na hizi pia ni katika dalili za kukaribia kwa Qiyaamah alizozitaja Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam).

Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) amesema: ((Katika dalili za kukaribia kwa Qiyaamah ni kupotea kwa elimu na kuongezeka ujinga.)) [Imepokewa na Al-Bukhaariy]


Kushindana Na Kujisifia Katika Kuipamba Misikiti

Imepokelewa kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:
((Katika dalili za kukaribia kwa Qiyaamah ni watu kushindana na kujisifia katika kuipamba misikiti.)) [Imepokewa na An-Nasaaiy]

Anasema Al-Bukhaariy: Amesema Anas (Radhiya Allaahu ‘Anhu) kuwa: “Watu wataipamba (Misikiti) lakini hawaendi kuswali ndani yake isipokuwa wachache”.

‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ‘Anhu) alikataza watu kuipamba sana Misikiti kwa sababu mapambo yanawababaisha watu ndani ya Swalah zao. Alipokuwa akisimamia utengenezaji wa Msikiti wa Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alikuwa akiwaambia wajenzi:
“Wakingeni watu na mvua na msitie rangi nyekundu wala manjano mkawababaisha watu”. [Imepokewa na Al-Bukhaariy]

“Mwenyezi Mungu Amrehemu ‘Umar bin Khattwaab (Radhiya Allaahu ‘Anhu)”, anasema Shaykh Yuusuf Al-Waabil, “kwani watu hawakutoshelezeka na kuwakinga watu na mvua wala hawakutoshelezeka na rangi za manjano na nyekundu, bali Misikiti siku hizi inapambwa na kujazwa nakhshi mfano wa nguo inavyonakshiwa”.


Mauaji

Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘Anhu) amesema kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) amesema: ((Qiyaamah hakitosimama mpaka ‘Haraj’ ikithiri.)) Wakamuuliza: “Ni nini hii ‘Haraj’ ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu?” Akasema: ((Mauaji, mauaji!.)) [Imepokewa na Muslim]

Na katika riwaya nyingine iliyosimuliwa na Abu Muusa (Radhiya Allaahu ‘Anhu) kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) amesema: ((Kabla ya Qiyaamah kusimama kutatokea ‘Haraj’.)) Wakamuuliza: “Ni nini hii ‘Haraj’ ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu?” Akasema: ((Mauaji)). Wakamuuliza: “Kuliko tunavyoua? Tunaua (vitani) katika mwaka mmoja zaidi ya alfu sabini?” Akasema: ((Si kama kuuwa kwenu washirikina, bali huko ni kuuana nyinyi wenyewe kwa wenyewe.)) Wakasema: “Tutakuwa na akili zetu siku hiyo?” Akasema: ((Zitaondolewa akili za wengi wa watu wa zama hizo. Watakuwa na wafuasi wengi kama vumbi, wengi wao watadhani kuwa wameshika chochote (katika haki), lakini (ukweli ni kuwa) hawana chochote.)) [Imepokewa na Imaam Ahmad na Ibn Maajah]

Halikadhalika, imesimuliwa kutoka kwa Abu Hurayrah kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) amesema: ((Naapa kwa Yule ambaye nafsi yangu imo mikononi mwake, haitotoweka dunia mpaka iwajie watu siku ambayo ndani yake muuaji hatojua kwa ajili gani ameua na wala aliyeuliwa kwa ajili gani ameuliwa.)) Akaulizwa: “Yatakuwaje hayo?” Akasema: ((Al-Haraj! aliyeuwa na aliyeuliwa (wataingia) Motoni.))

Haya yote yashatokea kweli katika zama zilizopita na tunayaona yakitokea katika zama zetu hizi pia. Hasa baada ya kuvumbuliwa kwa silaha zinazoangamiza.

Na katika Hadiyth sahihi iliyomo katika Mustadrak ya Al-Haakim, Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) amesema: ((Ummah wangu ni Ummah utakaohurumiwa, hawatokuwa na adhabu huko Akhera, kwani adhabu zao ni za dunia, mauaji na mashaka na mitetemeko.))


Mtu Atatamani Kufa

Imepokelewa kuwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘Anhu) amesema kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) amesema: ((Hakitosimama Qiyaamah mpaka mtu atakapopita penye kaburi la mtu akasema: “Yareti mimi ndiye ningelikuwa mahali pake”.)) [Imepokewa na Al-Bukhaariy]

Na kutoka kwa Abu Hurayrah pia, kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) amesema: ((Naapa kwa yule ambaye nafsi yangu imo mikononi Mwake, dunia haitotoweka mpaka mtu atakapopita penye kaburi akasimama na kusema: ‘Yareti ningelikuwa mimi ndani ya kaburi hili”. Si kwa ajili ya Dini, bali kwa ajili ya mitihani.)) [Imepokewa na Al-Bukhaariy]

Amesema Ibni Mas’uud (Radhiya Allaahu ‘Anhu): “Utakupitikieni wakati, mtu akiyakuta mauti yanauzwa, basi atayanunua”.

Wanasema Ma’ulamaa kuwa mambo kama haya si lazima yatokee katika kila nchi. Lakini yanaweza kutokea katika zama mbali mbali kutokana na mitihani mizito mbali mbali. Mtu anapokumbwa na mitihani hiyo atakapopita makaburini atahisi kama kwamba yule aliyelala ndani mule ndiye aliyestarehe. Ama yeye anajiona yumo katika adhabu, misukosuko mashaka na mitihani mikubwa isiyomalizika.


Kupigana Na Warumi (Wakiristo)

Kutoka kwa ‘Awf bin Maalik Al-Ashjaiy (Radhiya Allaahu ‘Anhu) amesema kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) amesema: ((Hesabu mambo sita, lazima yatatokea kabla ya kusimama Qiyaamah, miongoni mwa mambo sita hayo akasema: Kisha vita vitasimamishwa baina yenu na watu wa manjano (Wakiristo), kisha watakufanyieni khiana, watakujieni chini ya bendera themanini, chini ya kila bendera (watu) elfu kumi na mbili.)) [Imepokewa na Al-Bukhaariy]

Siku moja alikuja mtu kwa ‘Abdullaah bin Mas’uud (Radhiya Allaahu ‘Anhu) akamwambia: “Ewe ‘Abdullaah! Qiyaamah kitasimama (karibu sana)”. ‘Abdullaah bin Mas’uud (Radhiya Allaahu ‘Anhu) aliyekuwa amekaa akiwa ameegemea, akakaa vizuri kisha akamwambia: “Hakika ya Qiyaamah hakitosimama mpaka kwanza mirathi isigawiwe na ngawira isifurahiwe”.

Kisha akasema huku akiashiria upande wa Shaam (upande wa Mashariki): “Maadui watajikusanya kuwapiga vita Waislam, na Waislam watajikusanya kwa ajili ya kupambana nao”. Nikamuuliza: “Warumi? (Wakristo?)” Akasema: “Ndiyo, na katika vita hivyo wengi watartaddi, na Waislamu watatayarisha jeshi litakalokuwa tayari kufa lisilokubali kurudi nyuma bila ushindi, watapigana vita mpaka usiku utakapoingia, kisha watarudi nyuma hawa na wale, hapana mshindi kati yao, kisha jeshi litaangamia. Kisha Waislamu watatanguliza jeshi (lingine) litakalokuwa tayari kufa, watapigana vita mpaka wakati wa jioni, kisha watarudi nyuma hawa na wale, hapana mshindi kati yao, kisha litaangamia jeshi. Itakapoingia siku ya nne, Waislamu waliobaki watakuja kuwasaidia, na Mwenyezi Mungu Atawajaalia ushindi uwe upande wao, watapigana vita visivyopata kuonekana namna yake, hata ndege akipita juu yao, basi ataanguka akiwa amekufa”. [Imepokewa na Muslim]


Kuja Kwa Qahtwaaniy

Imepokelewa kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) amesema: ((Hakitosimama Qiyaamah mpaka kwanza aje mtu kutoka kabila la Qahtwaan (kabila la watu wa Yemen), atawaongoza watu kwa bakora (yaani atawaongoza na wataongoka vizuri na wote watampenda).)) [Imepokewa na Imaam Ahmad, Al-Bukhaariy na Muslim]

Imetayarishwa na Muhammad Faraj Salem Al Saiy

0 comments:

Post a Comment

Powered by Blog - Designer