Saturday, August 8, 2015

MCHUNGAJI ABDILI DINI NA KULIFANYA KANISA KUWA MSIKITI NCHINI NIGERIA .

Mchungaji mmoja nchini Nigeria sanjari na kuligeuza kanisa lake kuwa msikiti, ametamka shahada mbili na kuwa mfuasi wa dini Tukufu ya Kiislamu. 


Adekunle Afolabi ambaye amesilimu na kuwa Mwislamu anasema kuwa, amechukua uamzi huo baada ya kuota ndoto ya maajabu wakati alipokuwa katika maandalizi ya kufanya sherehe za kila mwaka za tangu kuasisiwa kanisa lake hilo lililokuwa likiitwa Apata Adura Cherubim katika mji wa Ado Ekiti jimbo la Ekiti. Kwa mujibu wa Afolabi ambaye kwa sasa anaitwa kwa jina la Alfa Abubakar Afolabi, akiwa usingizini, alijiwa na mtu aliyekuwa amevalia mavazi meupe, alimkinaisha kwamba dini ya Kiislamu ndio dini pekee inayoweza kumuokoa mwanadamu na kumfikisha peponi. Afolabi mwenye umri wa miaka 45, aliasisi kanisa lake hilo miaka mitano iliyopita. Anasema kuwa, tangu alipokuwa na umri wa miaka 25 alikuwa akijishughulisha na shughuli za uhubiri wa dini ya Kikristo na kusisitiza kuwa, kuanzia sasa ameamua kubadili dini na kuwa Mwislamu na kwamba atafariki dunia akiwa katika dini hiyo. Baada ya kuligeuza kanisa hilo na kulifanya kuwa msikiti, Afolabi amemteua sheikh mmoja wa mji huo kuendesha ibada za Kiislamu eneo hilo huku yeye akijikita katika kujifunza mafundisho ya dini ya Kiislamu hususan Qur’an Tukufu. Nigeria ni nchi yenye watu milioni 140 ambapo Waislamu ni asilimia 55 huku Wakristo wakiunda asilimia 40 ya raia hao. Katika baadhi ya maeneo jamii za Waislamu na Wakristo zinaishi kwa amani na ushirikiano, huku katika maeneo mengine zikiishi kwa mivutano inayotokana na migogoro ya kikaumu na kidini ambayo inasababishwa na watu wenye misimamo ya kufurutu ada.
CHANZO:SAUTI YA TEHRANI 

0 comments:

Post a Comment

Powered by Blog - Designer