Sifa zote njema Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wasallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Haifai kabisa kufupisha thanaa kwa maana kumtukuza Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kwa kuandika (s.w.t). Au kufupisha Jalla Jalaahu kwa kuandika (J.J). Vile vile haifai kumswalia Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwa kuandika (s.a.w) au (s).
Pia, haifai hata kufupisha katika kuwataja Maswahaba ‘Radhwiya Allaahu ‘anhu’ (Radhi za Allaah ziwe juu yake) kwa kuandika (R.A.) badala yake.
Hali kadhalika kuongeza neno 'Ta'ala' kwenye Salaam kwa kusema 'Assalaamu 'Alaykum wa RahmatuLLaahi Ta'ala wa Barakaatuh', si jambo tulilofundishwa katika Salaam na hivyo ni bora mtu kuliepuka katika Salaam.
Wengine huona tabu kuandika kirefu na hivyo hufupisha maamkizi haya katika mawasiliano ya barua, maandikiano ya simu za mkononi (text messages) ambayo ndio yameenea sana katika zama zetu hizi, barua pepe (e-mail) kwa kuandika ima A.A, au A.A.W, au A.A.W.W.B. Wamekosa kutambua kwamba wanakosa fadhila kubwa za kuamkiana kikamilifu, jambo ambalo halimchukui mtu hata dakika moja kuandika kirefu 'Assalaamu 'Alaykum' au Assalaamu 'Alaykum wa RahmatuLLaahi wa Barakaatuh'.
Kufupisha thanaa kwa Allaah au kumswalia Mtume ni dalili ya kutokuonyesha heshima mbele ya Allaah na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Dalili ya mapenzi kwao ni mtu kutokudharau au kutokuona uvivu kumtukuza Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) au kumswalia Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ikiwa kwa kutamka au kuandika.
Watu wengine huwa wanafanya hivyo na wakijulishwa kutokufaa kufanya hivyo, hutoa hoja kuwa makatazo ni katika matamshi na si katika maandishi! Na hoja nyingine ni kuwa vitabu vingi vya Maulamaa kumeandikwa kwa ufupi kumswalia Mtume kama hivi (ص) Lakini watu hao ima kwa kutokuwa na maarifa ya kutosha na Taariykh na kutazama nyakati za Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Maswahaba ikiwa waliwahi kutumia njia hizo katika maandishi au la, wao hujikuta wanafanya kwa mazoea na kuiga! Tunajua sote kuwa Mtume alishawahi kutuma barua kadhaa kwa watu mbalimbali wakiwemo viongozi na wafalme, na pia Maswahaba kama Makhalifa walikuwa wakiwaandikia Ma-Gavana na wateule wao katika majimbo mbalimbali na hakuna popote pale utaona walikuwa wakifupisha Salaam au kumswalia Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).
Ama suala la Mashaykh kuchapisha au kuchapishiwa vitabu vyao kwa kufupishwa hivyo na mashirika ya uchapishaji, haina maana kuwa ni sahihi wao kufanya hivyo. Ima hawajalipitia vyema na kulitafiti suala hilo, au hazijawafikia hoja kuhusiana na kutokufaa kufanya hivyo. Kwa hiyo kufanya kwao hivyo sio hoja ya kufaa jambo hilo.
Itambulikane kwamba maamkizi ya Kiislamu ni ‘Ibaadah kwani ni maamrisho kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) kama Anavyosema:
((يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَدْخُلُوا بُيُوتًا غَيْرَ بُيُوتِكُمْ حَتَّى تَسْتَأْنِسُوا وَتُسَلِّمُوا عَلَى أَهْلِهَا ذَلِكُمْ خَيْرٌ لَّكُمْلَعَلَّكُمْ تَذَكَّرُونَ))
((Enyi mlioamini! Msiingie nyumba zisio nyumba zenu mpaka muombe ruhusa, na muwatolee Salaam wenyewe. Hayo ni bora kwenu mpate kukumbuka)) [An-Nuur: 27]
Pia Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipohamia Madiynah, mafunzo ya maamkizi ya Salaam yalikuwa ni katika mafunzo ya mwanzo kabisa kuwapa Maswahaba alipoyatoa katika khutbah zake za mwanzo huko. Mafunzo haya pia yanabainisha kuwa kuamkia kwa maamkizi ya Kiislamu ni jambo litakalomuingiza Muislamu katika makaazi ya Pepo:
((ايها الناس ،أفشوا السلام، وأطعموا الطعام، وصلّوا بالليل والناس نيام تدخلوا الجنة بسلام)) رواه الترمذي، حديث صحيح
((Enyi watu, toeni (amkianeni kwa) salaam, na lisheni chakula, na Swalini watu wanapolala (Tahajjud), mtaingia Peponi kwa amani)) [At-Tirmidhiy – Hadiyth Hasan]
Na Salaam hizo ili mtu apate daraja kubwa na ukamilifu wa thawabu, ni sharti iwe imetimia kwa ukamilifu wake kama ilivyofundishwa katika Hadiyth ifuatayo:
عن عمران بن حصين رضي الله عنهما قال :جاء رجل الى النبي صلى الله عليه وسلم فقال :"السلام عليكم" فرد عليه السلام ثمجلس فقال النبي صلى الله عليه وسلم: ((عشر)) ثم جاء رجل اخر فقال: "السلام عليكم ورحمة الله" فرد عليه فجلس فقال: ((عشرون)) ثم جاء رجل اخر فقال: "السلام عليكم ورحمة الله وبركاته" فرد عليه فقال ((ثلاثون)) رواه ابو داود والترمذي و قال حديث حسن
'Imraan bin Huswayn (Radhwiya Allaahu 'anhuma) amesimulia: "Mtu mmoja alikuja kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamuamkia: "Assalaamu 'Alaykum" (Mtume) akamrudishia (Salaam) kisha yule mtu akaketi. Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: ((Kumi)) [Kwa maana amepata thawabu kumi]. Kisha akaja mtu mwengine, akasema: "Assalaamu 'Alaykum wa RahmatuLLaah" Naye akamrudishia, kisha yule mtu akaketi, Mtume akasema: ((Ishirini)). Kisha akaja mtu mwingine akasema: "Assalaamu 'Alaykum wa RahmatuLLaahi wa Barakaatuh". Naye akamrudishia kisha akasema ((Thelathini)) [Imesimuliwa na Abuu Daawuud na At-Trimidhiy na akasema Hadiyth Hasan]
Ama kuhusu Fatwa za Wanavyuoni zipo nyingi na miongoni mwazo ni kama zifuatazo:
Shaykh ‘Abdul-‘Aziyz bin Baaz (Rahimahu Allaah):
“Kama ilivyoamrishwa kumswalia Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwenye Swalaah katika Tashahhud, na imeamrishwa katika kutoa khutbah, kuomba Du’aa na kuomba maghfira, baada ya Adhaan, wakati wa kuingia na kutoka Msikitini, na wakati wa kumtaja katika hali nyinginezo, hivyo basi ni muhimu zaidi kufanya hivyo katika kumtaja jina lake katika kitabu, barua, makala n.k. Hivyo basi imeamrishwa kuandika Swalah na Salaam kwa ukamilifu ili kutimiza amri ya Allaah Aliyotuamrisha na ili msomaji apate kukumbuka kutaja kumswalia Mtume anapoisoma. Hivyo tusiandike Swalah na Salaam kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwa kifupi kama kuandika (S) au (S.A.W.) n.k. au mfumo wowote ambao watu wanatumia kwa sababu inakwenda kinyume na maamrisho ya Allaah na Kitabu Chake Anaposema:
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا صَلُّوا عَلَيْهِ وَسَلِّمُوا تَسْلِيمًا ﴿٥٦﴾
56. Enyi walioamini mswalieni na msalimieni kwa mamkizi ya amani na kwa tasliymaa
[Al-Ahzaab 33:56]
Kamati Kuu Ya Kudumu Ya Kutoa Fatwa Saudi Arabia ikiongozwa na Shaykh ‘Abdul-‘Aziyz bin ‘Abdillaah bin Baaz:
Wametoa fatwa ifuatayo watu walipoulizwa kuhusu kufupisha kumswalia Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): “Sunnah ni kuandika ibara kikamilifu (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) kwani hivyo ni kama du’aa, na du’aa ni ‘Ibaadah (ikiwa kuandika) kama ilivyo katika kutamka. Hivyo kufupisha kutumia herufi (Swaad ص ) au herufi kama (Swaad-Laam-‘Ayn-Miym) sio du’aa wala ibada ikiwa imetajwa katika kutamka au maandishi. Kwa sababu kufupisha huko hakukutumiliwa na karne tatu za mwanzo ambazo Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amezishuhudia ubora wake.”
[Fataawaa Al-Lajnat Ad-Daa'imah #18770 (12/208-209)]
Al-Fayruuz ‘Abaadiy:
“Haipasi kutumia alama au vifupisho kuhusiana na Salaam kwa wanavyofanya baadhi ya wavivu na watu wajinga na pia baadhi ya wanafunzi wa elimu wanaoandika ‘Swaad-Laam-‘Ayn-Miym’ badala ya ‘Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam.”
[Katika Kitabu chake Asw-Swalaatu wal-Bushr, kama iliyvonukuliwa katika Mu'jam Al-Manaahiy Al-Lafdhwiyyah (Uk .351)
Ahmad Shaakir:
“Ni mila za upumbavu za karne za sasa kwamba watu wanafupisha kuandika Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam”
Ufafanuzi [Musnad Imaam Ahmad (#5088, 9/105)]
WasiyuLLaah Al-'Abbaas:
“Hairuhusiwi kufupisha Salaam kwa ujumla katika maandishi kama ilivokuwa hairuhusiwi kufupisha Swalah na Salaam kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa wa sallam).
[Jibu aliloandika Shaykh kwa mkono, Faili Namba: AAWA004, tarehe 24.06.1423]
Kadhalika si watu wote wanaoelewa vifupisho hivyo, na unapoandika hivyo utakuwa unamchanganya na kumshughulisha mtu yule kwa mambo kama hayo. Leo hii tunaona watu wengi wakisoma vitabu vya Kiswahili na hata tafsiri za Qur-aan za Kiswahili vilivyofupishwa sifa hizo, huwa wanazisoma hivyo hivyo kwa ufupi kama zilivyoandikwa! Mtu anapokutana na jina la Allaah na kusema ‘es dabliuu ti’ kwa sababu kumeandikwa kwenye kitabu (s.w.t.), au anaposoma jina la Mtume na kisha anasema ‘es ei dabliuu’ kwa sababu kumeandikwa (s.a.w.) kwenye vitabu hivyo!! Hivyo ni uvurugaji na pia kumkosea Allaah na Mtume Wake kwa kuwapa sifa za ajabu zisizowahusu, na makosa hayo huwarejea wale walioandika kuliko yule mwenye kusoma kwa kutokujua!
Hivyo basi haifai kufupisha kwani ni kujikosesha thawabu na fadhila zinazopatikana katika kutaja thanaa za Allaah na kumswalia Mtume na pia kutoa Salaam kwa ukamilifu, na pia ikiwa mtu atafikiwa na ufafanuzi huu na akaendelea kuifanya hayo, basi ni alama ya kiburi na huenda asikose tu thawabu za kuandika, bali huenda akapata na dhambi za kuifanyia haki kiburi na ujeuri.
Na Allaah Anajua zaidi
0 comments:
Post a Comment