Sunday, November 6, 2016

TAHIYYATUL MASJID NA SUNNATUL UDHUI


TAHIYYATUL MASJID

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kasema: “Yeyote miongoni mwenu atakapoingia Msikitini, hapaswi kukaa mpaka aswali rakaa mbili.” [Al-Bukhaariy na Muslim]
Jaabir (Radhiya Allaahu 'anhuma) kasema: “Mtu mmoja aliingia Msikitini siku ya Ijumaa wakati Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anatoa khutba, akamuuliza: "Je, umeswali?"
Akasema: "Hapana". Akasema (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): "inuka uswali rakaa mbili na uzifanye nyepesi " [Al-Bukhaariy na Muslim]
Tahiyyatul Masjid ni Swala ya kuuamkia Msikiti kwa kuupaheshima. Mtu anapoingia Msikitini jambo la kwanza anatakiwa aswali rakaa mbili hizi hata kama iwe ameingia kwa ajili ya dharura nyengine mbali mbali. Swala hii haizuiliwi na nyakati wala khutba wala mawaidha. Kinachoizuia Tahiyyatul Masjid ni kuqimiwa kwa Swala ya Fardhi au wakati Swala ya fardhi inaswaliwa, hapo hatoruhusiwa mtu kuendelea na Swala hii, bali anatakiwa aiwache kwa ajili ya kujiunga na Swala ya Fardhi.


SUNNATUL UDHUI

Ni Sunnah ya rakaa mbili inayoswaliwa baada ya kutia udhu.
Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kasema: “Mmoja wenu akishatia udhu vizuri kabisa halafu akaswali rakaa mbili kwa moyo wake wote na uso (mkamilifu), Pepo itakuwa ni yake” [Muslim, Abu Daawuud, Ibn Maajah na Ibn Khuzaymah]
Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kasema: “Yeyote atakaetia udhu sawasawa halafu akaswali rakaa mbili bila ya kuwa na mawazo yoyote akilini mwake, atasamehewa madhambi yake yote yaliyopita” [Al-Bukhaariy na Muslim]
Siku moja Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alimuuliza Bilaal (Radhiya Allaahu ‘anhu): "Nielezee juu ya amali njema kabisa unayoitenda, kwani nimesikia sauti ya viatu vyako ukiwa mbele yangu Peponi?" Bilaal (Radhiya Allaahu ‘anhu) akamjibu: "Ewe Mtume wa Alla sijafanya amali yoyote niliyoiona kuwa ni bora kwangu isipokuwa kawaida yangu mimi kila nikimaliza kutia udhu huswali kadiri ninavyojaaliwa kuswali”. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia: “Hilo ndilo lililokufikisha (Peponi)”. [Al-Bukhaariy]
TUNAMUOMBA ALLAH ATUWEZESHE KUZISIMAMISHA SWALA ZOTE KIKAMILIFU

0 comments:

Post a Comment

Powered by Blog - Designer