Inatupasa
tumshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'alaa) kwa neema Aliyotujaalia ya
kutuwekea miezi mitukufu, au siku tukufu au nyakati tukufu ambazo
vitendo vyake vyema huwa na thawabu nyingi sana. Na hivi tunakaribia
kabisa kuingia katika mwezi mwingine mtukufu wa Dhul-Hijjah. Katika
mwezi huu, siku kumi za mwanzo ni siku bora kabisa mbele ya Allaah
ambazo 'amali yoyote inayotendwa humo ni yenye kupendwa mno na Allaah:
عن ابن عباس رضي الله عنهما، أن النبي صلى الله عليه وسلم قال: ((مَا
مِنْ أَيَّامٍ الْعَمَلُ الصَّالِحُ فِيهَا أَحَبُّ إِلَى اللَّهِ مِنْ
هَذِهِ الْأَيَّامِ)) يَعْنِي أَيَّامَ الْعَشْرِ قَالُوا: يَا رَسُولَ
اللَّهِ وَلَا الْجِهَادُ فِي سَبِيلِ اللَّهِ؟ قَالَ: ((وَلَا الْجِهَادُ
فِي سَبِيلِ اللَّهِ إِلَّا رَجُلٌ خَرَجَ بِنَفْسِهِ وَمَالِهِ فَلَمْ
يَرْجِعْ مِنْ ذَلِكَ بِشَيْ)) البخاري
Imetoka
kwa Ibn 'Abbaas (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) kwamba Mjumbe wa Allaah
amesema: ((Hakuna siku ambazo vitendo vyake vyema Anavipenda Allaah kama
siku kumi hizi)) (siku kumi za mwanzo wa mwezi wa Dhul-Hijjah)
Akaulizwa, je, hata Jihaad katika njia ya Allaah? Akajibu (Swalla
Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ((Hata Jihaad katika njia ya Allaah
isipokuwa mtu aliyekwenda na nafsi yake na mali yake ikawa hakurudi na kimojawapo)) [Al-Bukhaariy]
Zifuatazo
ni fadhila kuu za masiku hayo kumi ya Dhul-Hijjah. Ee ndugu Muislamu!
Utakapojipwekesha katika 'ibaadah na kutenda amali njema zenye ikhlaasw
na zinazotokana na mafunzo Sahihi ya Sunnah za Mtume (Swalla Allaahu
‘alayhi wa aalihi wa sallam), basi bila shaka utajichumia thawabu
maradufu na ambazo zitakuwa nzito In Shaa Allaah katika mizani yako.
Allaah Ameziapia Siku Kumi Hizi
Kwa
jinsi zilivyokuwa na umuhimu mkubwa siku hizo kumi, hadi kwamba Allaah
(Subhaanah wa Ta'alaa) Ameziapia katika Qur-aan Anaposema:
بِسْمِ اللّهِ الرَّحْمَنِ الرَّحِيمِ ((وَالْفَجْرِ)) ((وَلَيَالٍ عَشْرٍ))
BisimiLLaahir-Rahmaanir-Rahiym. ((Naapa kwa Alfajiri)) ((Na kwa masiku kumi)) [Al-Fajr: 1-2]
Wanachuoni wafasiri wa Qur-aan wamekubaliana kwamba zilokusudiwa hapo ni Siku kumi za Dhul-Hijjah.
Siku Za Manufaa Na Kumkumbuka Allaah
Inapasa kumdhukuru mno Allaah (Subhaanah wa Ta’alaa) kwa kukumbuka Neema Zake zisizohesabika:
((لِيَشْهَدُوا مَنَافِعَ لَهُمْ وَيَذْكُرُوا اسْمَ اللَّهِ فِي أَيَّامٍ مَّعْلُومَاتٍ))
((Ili washuhudie manufaa yao na kulitaja Jina la Allaah katika siku zinazojulikana)) [Al-Hajj: 28]
Ibn
‘Abbaas (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) kasema: “Hizo ni siku kumi za
Dhul-Hijjah”. Na Amesema: “Manufaa ya dunia hii na ya Aakhirah” .
Manufaa ya Akhera yanajumuisha kupata Radhi za Allaah. Manufaa ya vitu
vya dunia inajumuisha wanyama wa kuchinjwa na biashara. [Tafsiyr Ibn
Kathiyr]
'Amali Zake Ni Bora Kuliko Kwenda Katika Jihaad Fiy SabiliLLaah
Kutokana
na ilivyotajwa katika usimulizi wa Hadiyth ifuatayo, kwamba amali
yoyote utendayo katika masiku kumi hayo, ni bora kuliko kwenda kupigana
jihadi vitani. Ukizingatia kwenda kupigana Jihaad ni jambo zito mtu
kuliitikia, kwani huko kuna mashaka mbali mbali, ikiwemo khofu ya
kujeruhiwa na kupoteza viungo vya mwili, kufariki, kupoteza mali n.k.
Ila hilo si zito kwa mwenye imani ya hali ya juu kabisa kutaka
kuyakabili mashaka hayo na kutamani kufa shahidi. Kwa hiyo usidharau
amali yoyote hata iwe ndogo vipi itekeleze kwani Allaah (Subhaanahu wa
Ta'alaa) ni Al-Jawwaad (Mwingi Wa Ukarimu), Al-Kariym (Karimu),
Al-Wahhaab (Mwingi Wa Kutunuka, Mpaji Wa Yote), Al-Majiyd (Mwingi Mno Wa
Vipawa Na Ukarimu).
عن ابن عباس رضي الله عنهما، أن النبي صلى الله عليه وسلم قال:)) ما من أيام العمل الصالح فيها أحب إلى الله من هذه الأيام)) - يعني أيام العشر-. قالوا: يا رسول الله، ولا الجهاد في سبيل الله ؟ قال: ((ولا الجهاد في سبيل الله، إلا رجل خرج بنفسه وماله ثم لم يرجع من ذلك بشيء)) البخاري
Imetoka
kwa Ibn 'Abbaas (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) kwamba Mjumbe wa Allaah
amesema: ((Hakuna siku ambazo vitendo vyake vyema Anavipenda Allaah kama
siku kumi hizi)) (siku kumi za mwanzo wa mwezi wa Dhul-Hijjah)
Akaulizwa, je, hata Jihaad katika njia ya Allaah? Akajibu (Swalla
Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ((Hata Jihaad katika njia ya Allaah
isipokuwa mtu aliyekwenda na nafsi yake na mali yake ikawa hakurudi na kimojawapo)) [Al-Bukhaariy]
'Ibaadah Zote Zimejumuika Katika Siku Hizi
'Ibaadah zote zimejumuika katika siku kumi hizi nazo ni Swalah, Swawm, Swadaqah, Hajj, wala hazijumuiki hizi wakati mwingine.
Vitendo Vyema Vya Kutenda Katika Siku Kumi Hizi
1- Kutekeleza Hajj na 'Umrah (kwa mwenye uwezo)
عن أبي هريرة رضي الله عنه أن رسول الله صلى الله عليه وسلم قال ((العمرة إلى العمرة كفارة لما بينهما. والحج المبرور ليس له جزاء إلا الجنة)) أخرجه البخاري و مسلم
Imetoka
kwa Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Mtume (Swalla Allaahu
'alayhi wa aalihi wa sallam) kasema: (('Umrah hadi 'Umrah hufuta
(madhambi) baina yake, na Hajjum-Mabruwr haina jazaa ila Pepo)) [Al-Bukhaariy na Muslim]
عن أبي هريرة رضي الله عنه قال: "سئل رسول الله صلى الله عليه وسلم: أي الأعمال أفضل؟ قال: ((إيمان بالله ورسـوله)). قيل: ثم مـاذا؟ قال: ((الجهاد في سبيل الله)) قيل: ثم ماذا؟ قال: ((حج مبـرور)) متفق علية
Imetoka
kwa Abu Hurayrah(Radhwiya Allaahu 'anhu) ambaye amesema: "Aliulizwa
Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amali gani ni bora
kabisa?" Kasema: ((Kumuamini Allaah na Mtume Wake)), Akaulizwa:"Kisha
nini?" Kasema: ((Jihaad katika njia ya Allaah)). Akaulizwa: "Kisha
nini?" Kasema: ((Hajj Mabruwr)) [Al-Bukhaariy na Muslim]
2- Kuomba Tawbah ya kweli na kujiepusha na maasi
Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'alaa):
(( يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا تُوبُوا إِلَى اللَّهِ تَوْبَةً نَّصُوحًا))
((Enyi mlioamini! Tubuni kwa Allaah tawbah iliyo ya kweli!)) [At-Tahriym: 8]
Na
Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ametupa matumaini
makubwa ya kufutiwa madhambi na makosa yetu katika usimulizi ufuatao:
عن أنس رضي الله عنه قال: سمعت رسول الله صلى الله عليه وسلم يقول: ((قال الله: يا ابن آدم إنك ما دعوتني ورجوتني غفرت لك على ما كان منك ولا أبالي، يا ابن آدم لو بلغت ذنوبك عنان السماء، ثم استغفرتني غفرت لك ولا أبالي، يا ابن آدم إنك لو أتيتني بقراب الأرض خطايا، ثم لقيتني لا تشرك بي شيئاً لأتيتك بقرابها مغفرة)) أخرجه الترمذي وحسنه الألباني في الصحيحة
Kutoka
kwa Anas (Radhwiya Allaahu 'anhu): "Nimemsikia Mtume (Swalla Allaahu
'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: ((Allaah Amesema: Ee Mwana Adam!
Hakika ukiniomba na ukanitaraji (kwa malipo) Nitakusamehe yale yote
uliyonayo na wala Sijali, Ee Mwana Aadam! Lau zingefikia dhambi zako
ukubwa wa mbingu, kisha ukaniomba maghfira, Ningekughufuria bila ya
kujali (kiasi cha madhambi uliyoyafanya). Ee Mwana Aadam, Hakika
ungenijia na madhambi yakaribiayo ukubwa wa ardhi, kisha ukakutana nami
na hali hukunishirikisha chochote, basi Nami Nitakujia na msamaha
unaolingana nao)) [Imetolewa na At-Tirmidhiy na Shaykh Al-Albaaniy kaipa daraja ya Hasan]
3- Kumkumbuka sana Allaah (Subhaanahu wa Ta'alaa)
Kwa Tasbiyh, Tahmiyd, Tahliyl, Takbiyr (kusema: Subhaana Allaah, AlhamduliLlaah, Laa Ilaaha Illa Allaah, Allaahu Akbar)
عن ابْنِ عُمَرَ عَنِ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَال: (( مَا مِنْ أَيَّامٍ أَعْظَمُ عِنْدَ اللَّهِ وَلَا أَحَبُّ إِلَيْهِ مِنَ الْعَمَلِ فِيهِنَّ مِنْ هَذِهِ الْأَيَّامِ الْعَشْرِ فَأَكْثِرُوا فِيهِنَّ مِنَ التَّهْلِيلِ وَالتَّكْبِيرِ وَ التَّحْمِيدِ )) أخرجه أحمد
Imetoka
kwa Ibn 'Umar (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) kwamba Mtume (Swalla Allaahu
'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Hakuna siku zilizokuwa tukufu
kwa Allaah na zilizokuwa vitendo vyake vipenzi kabisa Kwake kama siku
hizi, basi zidisheni Tahliyl na Takbiyr na Tahmiyd)) [Ahmad]
Inavyopasa kufanya Takbiyr:
الله أكبر. الله أكبر. لا إله إلا الله. والله أكبر. الله أكبر ولله الحمد
“Allaahu Akbar, Allaahu Akbar, Laa Ilaaha Illa Allaah Wa-Allaahu Akbar, Allaahu Akbar WaliLLaahil-Hamd”
Takbiyr hii ni aina mbili:
Takbiyratul-Mutwlaq - Za Nyakati Zote
Takbiyr
wakati wote usiku au mchana tokea Magharibi unapoingia tu mwezi wa
Dhul-Hijjah na inaendelea mpaka siku ya mwisho ya Tashriyq (tarehe 13
Dhul-Hijjah) inapoingia Magharibi.
Takbiyratul-Muqayyad - Za Nyakati Maalumu
Takbiyr kuanzia Alfajiri ya siku ya 'Arafah mpaka inapoingia Magharibi ya siku ya mwisho ya Tashriyq.
4- Kufufua Sunnah ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)
Wanaume
wanatakiwa waseme kwa sauti ili kuwakumbusha wengine na kufufua Sunnah
ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na wanawake waseme kimya kimya isipokuwa wakiwa na mahaarim wao. Kufufua Sunnah ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ni
muhimu kwani bila ya kufanya hivyo tutakuwa kwanza tunakosa fadhila
zake, pili zitapotea Sunnah za kipenzi chetu Mtume (Swalla Allaahu
'alayhi wa aalihi wa sallam).
Mtume
(Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kasema: ((Atakayemuongoza
mwenzake kufanya jambo jema atapata thawabu sawa sawa na za yule
atakayetenda hilo jambo jema)) [Muslim]
كان ابن عمر وأبو هريرة رضي الله عنهما يخرجان إلى السوق في أيام العشر يكبران، ويكبر الناس بتكبيرهما (البخاري)
Ibn
'Umar na Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) walikuwa wakienda
sokoni katika siku kumi na kufanya Takbiyr kwa sauti na watu
wakiwaigiza)) [Al-Bukhaariy]
5- Kufunga siku hizi khaswa siku ya 'Arafah
Kufunga siku hii ni kufutiwa madhambi ya miaka miwili:
عَنْ أَبِي قَتَادَةَ رضي الله عنه أن النَّبِيَّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((صِيَامُ يَوْمِ عَرَفَةَ أَحْتَسِبُ عَلَى اللَّهِ أَنْ يُكَفِّرَ السَّنَةَ الَّتِي قَبْلَهُ وَالسَّنَةَ الَّتِي بَعْدَهُ )) أخرجه مسلم
Imetoka kwa Abu Qataadah (Radhwiya Allaahu 'anhu) ambaye amesema: Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kasema: “Swawm ya 'Arafah nataraji (kwa Allaah) kufuta madhambi ya mwaka uliopita na wa baada yake.” [Muslim]
Swawm pia ni kuwekwa mbali na Moto.
عن أبي سعيد الخضري رضي الله عنه قال: قال عليه الصلاة والسلام ((من صام يوما في سبيل الله باعد الله وجهه عن النار سبعين خريفا) رواه البخاري ومسلم
Kutoka
kwa Abu Sa'iydil-Khudhwriyy (Radhwiya Allaahu 'anhu) ambaye amesema:
Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kasema: ((Mwenye
kufunga siku kwa ajili ya Allaah, basi Allaah Atamuokoa uso wake
kutokana na moto kwa umbali wa miaka sabini)) [Al-Bukhaariy na Muslim]
Na Swawm piia ina thawabu maradufu.
قال صلى الله عليه وسلم: (( كل عمل ابن آدم له الحسنة بعشر أمثالها إلى سبعمائة ضعف. يقول الله عز وجل: إلا الصيام فإنه لي وأنا أجزي به)) أخرجه البخاري ومسلم
Amesema
Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ((Kila 'amali njema
ya mwanaadamu inalipwa mara kumi na inaongezewa thawabu kutoka kumi hadi
mia saba, na Allaah Anasema isipokuwa Swawm, kwani hiyo ni kwa ajili
Yangu na Mimi Ndiye nitakayemlipa)) [Al-Bukhaariy na Muslim]
6- Kuzidisha vitendo vyema mbali mbali
Mbali
ya kutekeleza fardhi ya Swalah kwa kuswali kwa wakati wake, kuswali
Sunnah zaidi, kusoma Qur-aan, Swadaqah, Du'aa, kutii wazazi na
kuwafanyia wema, kuwasiliana na jamaa (kuunga undugu), kuwafanyia wema
jirani, kuamrishana mema na kukatazana maovu, kufanyiana wema na ihsani
na kadhalika.
7- Kuchinja baada ya Swalah ya 'Iyd
Anasema Allaah (Subhaanahu Wa Ta'alaa):
((فَصَلِّ لِرَبِّكَ وَانْحَرْ))
((Basi Swali kwa ajili ya Mola wako na uchinje)) [Al-Kawthar: 2]
Pia, usimulizi ufuatao tunapata maelezo ya aina ya mnyama wa kuchinja na uchinjaji wake.
فعَنْ أَنَسٍ رضي الله عنه قَالَ: (( ضَحَّى النَّبِيُّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ بِكَبْشَيْنِ أَمْلَحَيْنِ أَقْرَنَيْنِ ذَبَحَهُمَا بِيَدِهِ وَسَمَّى وَكَبَّرَ وَوَضَعَ رِجْلَهُ عَلَى صِفَاحِهِمَا )) متفق عليه
Imetokea
kwa Anas (Radhwiya Allaahu 'anhu) ambaye amesema: "Mtume (Swalla
Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alichinja kondoo wawili weupe*
wenye pembe, amewachinja kwa mikono yake, akasema BismiLLaah na Allaahu
Akbar na akaweka mguu wake upande wa nyuma yao". [Al-Bukhaariy na Muslim]
*Baadhi ya Wanachuoni wamesema kuwa ni weupe ulio na alama nyeusi, wengine wamesema uliochanganyika na wekundu.
Kitendo
hiki cha kuchinja ni 'Ibaadah tukufu na ni Sunnah iliyosisitizwa hata
wanachuoni wameona kuwa ni Waajib kwa kila aliyekuwa na uwezo wa
kuchinja.
Yanayompasa kufanya mwenye kutaka kuchinja
Baada
ya kutia niyyah ya kuchinja, asikate mtu nywele wala kucha mpaka amalize
kuchinja kama tulivyoamrishwa katika Hadiyth ifuatayo:
عن أم سلمة رضي الله عنها، أن النبي صلى الله عليه وسلم قال: (( إذا رأيتم هلال ذي الحجة وأراد أحدكـم أن يضحّي فليمسك عــن شعره وأظفاره))، وفي راوية ((فلا يأخذ من شعره ولا من أظفـاره حتى يضحّي)) مسلم
Imetoka kwa Ummu Salamah (Radhwiya Allaahu 'anhaa) kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Ukiandama mwezi wa Dhul-Hijjah na ikiwa yuko anayetaka kuchinja basi azuie (asikate) nywele zake na kucha zake).
Na katika riwaya nyingine ((Asikate nywele wala kucha mpaka akimaliza kuchinja)) [Muslim na wengineo]
Hii ni fadhila na neema kwetu maana tunakuwa katika hali ya ‘Ihraam’ kama waliokuwa kwenye Hijjah. Ikiwa amesahau mtu, mfano akakata kucha basi aendelee tu na niyyah yake mpaka amalize kuchinja.
8- Kuhudhuria Swalah ya 'Iyd
Mtume
(Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amewahimiza mpaka wanawake
walio katika hedhi na wazee waende kusikiliza khutbah ya Swalah. Wakati
wa Swalah ukifika, wanawake hao wenye hedhi wajitenge kando hadi
itakapomalizika Swalah na kisha wajiunge na wenzao kusikiliza khutbah.
Siku Ya ‘Arafah Ni Siku Ya Tisa Dhul-Hijjah
a) Madhambi ya miaka miwili hufutiwa atakayefunga
Siku hii tukufu ni siku iliyokamilika Dini yetu. Thawabu za kufunga siku hii ni kufutiwa madhambi ya miaka miwili.
عَنْ أَبِي قَتَادَةَ رضي الله عنه أن النَّبِيَّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((صِيَامُ يَوْمِ عَرَفَةَ أَحْتَسِبُ عَلَى اللَّهِ أَنْ يُكَفِّرَ السَّنَةَ الَّتِي قَبْلَهُ وَالسَّنَةَ الَّتِي بَعْدَهُ )) أخرجه مسلم
Imetoka kwa Abu Qataadah (Radhwiya Allaahu 'anhu) ambaye amesema: Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kasema kuhusu Swawm ya 'Arafah kuwa ((inafuta madhambi ya mwaka uliopita na wa baada yake)) [Muslim]
b) Siku ambayo huachiliwa watu wengi huru na moto
عن عائشة رضي الله عنها أن رسول الله صلى الله عليه وسلم قال: ((ما من يوم أكثر من أن يعتق الله فيه عبداً من النار من يوم عرفة)) رواة مسلم
Imetoka
kwa Mama wa Waumini, 'Aaishah (Radhwiya Allaahu 'anhaa) kwamba Mtume
(Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Hakuna siku
Allaah Anayowaacha huru waja na moto kama siku ya ‘Arafah)) [Muslim]
c) Du'aa bora kabisa ni Du'aa katika siku ya 'Arafah
Vile vile inapasa kumtaja sana Allaah siku hii kama alivyosema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa:
((خير الدعاء دعاء يوم عرفة، وخير ما قلت أنا والنبيون من قبلي: لا إله إلا الله وحده لا شريك له، له الملك وله الحمد وهو على كل شيء قدير)) روى الترمذي
((Du’aa bora kabisa ni du’aa katika siku ya 'Arafah, na yaliyo bora kabisa niliyosema mimi na Mitume kabla yangu ni:
'Laa Ilaaha Illa Allaah Wah-dahu Laa Shariyka Lahu, Lahul-Mulku Wa-Lahul-hamdu Wa Huwa 'Alaa Kulli Shay-in Qadiyr’)) [At-Tirmidhiy]
Siku Ya Kuchinja Ni Siku Kuu Ya ‘Iyd
Kasema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):
((إن أعظم الأيام عند الله يوم النحر، ثم يوم الْقَرّ)) سنن أبي داود
((Siku iliyo tukufu kabisa kwa Allaah ni siku ya kuchinja, kisha siku ya kutulia)) (yaani siku ya kukaa Minaa) [Abu Daawuwd]
Siku Za Tashriyq
Ni
siku ya kumi na moja na kumi na mbili na kumi na tatu ya Dhul-Hijjah
yaani baada ya siku ya 'Iyd. Na siku hizi tatu zimeitwa siku za Tashriyq
kwa sababu watu walikuwa wakikatakata nyama na kuzianika juani. Siku za
kuanika (nyama) juani. Na pi siku hizi hujulikana kwa 'siku za Minaa'.
a) Kumkumbuka sana Allaah
Katika siku hizi inampasa Muislamu azidishe kumkumbuka Allaah (Subhaanahu wa Ta'alaa) kama Anavyosema:
((وَاذْكُرُواْ اللّهَ فِي أَيَّامٍ مَّعْدُودَاتٍ))
((Na mtajeni Allaah katika zile siku zinazohisabiwa)) [Al-Baqarah: 203]
Ibn
'Abbaas (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) kasema: Siku zinazohisabiwa ni siku
za Tashriyq (11, 12, 13 Dhul-Hijjah) na Siku zinazojulikana ni siku za
kumi za mwanzo za Dhul-Hijjah. [Al-Qurtwubiy: 3.3]
b) Haifai kufunga katika siku hizi
Haifai kufunga katika siku hizi hata kama mtu alikuwa na mazowea ya kufunga Sunnah za Jumatatu na Alkhamiys au Ayyaamul-Biydh kutokana na makatazo kama haya:
عن
أبي هريرة أن رسول الله صلى الله عليه وسلم بعث عبد الله بن حُذافة يطوف
في منى: ((لا تصوموا هذه الأيام، فإنها أيام أكل وشرب، وذكر الله، عز وجل))
Imetoka
kwa Abu Hurayrah kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa
sallam) alimtuma 'Abdullaah bin Hudhaafah azunguke Minaa na atangaze
"Msifunge siku hizi, kwani hizi ni siku za kula na kunywa na kumkumbuka
Allaah Mwenye Nguvu Mtukufu' [At-Twabariy 4: 211]
Tunamuomba
Allaah (Subhaanahu wa Ta'alaa) Atupe umri na afya na uwezo wa kuweza
kufanya mengi ya kumridhisha katika siku hizi tukufu na siku zote
nyingine ili tujipatie thawabu nyingi na Atujaaliye tuwe katika wale
wanaosikiliza kauli na daima wakafuata zile zilizo njema. Aamiyin